Makala

MKASA WA SOLAI: Siasa zachelewesha fidia kwa waathiriwa

May 14th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wa Solai katika Kaunti ya Nakuru wameadhimisha mwaka mmoja tangu mkasa wa mafuriko uwapate ambapo watu 48 walipoteza maisha yao.

Mwaka uliopita bwawa la Patel lilivunja kingo zake na kusomba vijiji, mifugo, nyumba, mali, pamoja na shule zinazopatikana katika eneo la Solai.

Cha kushangaza ni kuwa japo wakazi wa Solai waliadhimisha siku hiyo kwa njia ya kipekee, wanasiasa hawakuwepo kuwatia moyo maishani, jambo linaloibua maswali kuhusu uongozi katika kaunti hiyo.

Bi Rose Wangoi aliyepoteza watoto wanne aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa anaukumbuka mkasa huo kama jinamizi lililomwachia machungu ya muda mrefu ambayo hayawezi kufutika kutoka kwenye kumbukumbu zake.

Anakumbuka vyema siku ya mkasa ambapo bwawa la Solai lilipasuka na kuwangaamiza watu zaidi ya 48, saa chache baada ya giza kuingia wakati shughuli zikiendelea mtaani kama kawaida.

Anasema maeneo yaliyopata pigo zaidi ni Nyakenyua, Endago, Maiminet na Arutani ambapo shirika la Msalaba Mwekundu lililazimika kuleta chakula cha msaada na dawa kuwahudumia waathiriwa.

Kilimo

“Tangu mkasa huo ufanyike, mchanga katika eneo la Solai ulisombwa na kubakisha mawe ambayo hayawezi kukuza mimea inayotegemewa na wakazi wa hapa, wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema.

Anasema shirika la Msalaba Mwekundu lilitoa msaada wa jumla ya nyumba 37, kwa wahanga wa mkasa huo ambapo yeye hakuwa mmoja wao.

Kulingana na Rose, mumewe alikataa wahamie nyumba mpya kwa sababu eneo hili limekuwa likimpatia kumbukumbu mbaya za kuwapoteza watoto wake wote.

Rose Wangoi, mama aliyepoteza watoto wote wanne katika mkasa wa Solai sasa amejaliwa mtoto mwingine. Picha/ Richard Maosi

Hata hivyo, anaamini kuwa kuna kundi la wamiliki wa nyumba za kupanga ambao bado hawajapatiwa fidia kwa sababu pia walipatwa na hasara, kwa njia moja au nyingine.

Pia anaamini idadi ya watu waliopoteza maisha yao ni kubwa kuliko ile iliyotolewa na serikali kwani zaidi ya watu 5,000 walipoteza makao yao.

Imekuwa vigumu kwa wamiliki wa nyumba kuendelea na hali yao ya maisha kwa sababu ya hasara kubwa waliyokadiria.

Wengine walilemewa na msongo wa mawazo, wakaamua kujiingiza katika mihadarati ili kuepuka kumbukumbu za mkasa huo.

“Nawafahamu waathiriwa zaidi ya 20 waliokuwa wakiishi hapa, walipoteza wapendwa wao na kupoteza mali lakini hawajapokea fidia mpaka sasa,” aliongezea.

Japo alipoteza watoto wake wote wanne, anasema amejaliwa mtoto mwingine ambaye angalau amemsaidia kupoza kovu la moyoni.

Mbali na wakazi wa Solai kupatiwa fidia, anaona ni afadhali wawezeshwe kurejelea maisha ya kawaida ili waendelee kutekeleza kilimo cha mahindi na viazi kama awali.

Bw Maina Muhia, mwenyekiti wa wakazi walioadhiriwa anasema maafisa wa Msalaba Mwekundu walikuwa wakishirikiana na kanisa la AIC kutengeneza nyumba kwa wale waliopata hasara.

Siasa

Lakini tangu swala la siasa liingizwe katika fidia, wakazi wamekuwa wakifaidika nusunusu.

Anasikitika kwa sababu wakazi hawawezi kuendeleza shughuli za kilimo, kwa sababu ya mawe yaliyobakia kwenye mashamba yao.

“Tunafurahi kuona hatua ya kuwajengea nyumba watu 37 inaendelea, lakini kilichobakia ni kuhakikisha watu wetu wanarejelea shughuli zao za kila siku,” Bw Muhia alisema.

Mary Waruguru mfanyikazi wa kijamii ambaye amekuwa akiwapa ushauri nasaha waathiriwa wa mkasa wa Solai. Picha/ Richard Maosi

Kabla ya mkasa eneo la Solai lilikuwa likizalisha chakula cha kutosha kama vile mahindi, nyanya na maharagwe lakini sasa hawawezi kwa sababu maji yalibeba mchanga wote wenye rutuba.

Mwenyekiti huyo wa wakazi anasema eneo lililopata hasara ni kilomita 15 kutoka kwenye eneo la kwenye shule ya msingi ya Nyakinyua ambapo dhoruba ilianzia.

Bw Muhia anasema pia shirika la haki za kibinadamu liliwasaidia wakazi kutengeneza kisima cha maji katika eneo la Nyakinyua.

Shule ya msingi ya Nyakinyua iliyobebwa na maji pia imetengenezwa na Bw Patel mwenyewe na masomo kurejelea hali ya kawaida mwaka mmoja baada ya mkasa.

Kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya Power na ile ya Safaricom pia ziliingia kati kunusuru hali baada ya milingoti ya stima na ile ya mawimbi ya simu kusombwa na maji.

Kulingana na kamishna wa haki za kibinadamu George Kegoro, kuwafidia waathiriwa ndio njia ya kipekee itakayofanya wafahamu kuwa wametendewa haki.