Habari

MKASA: Wabunge waliweka lawamani shirika la huduma za feri

October 2nd, 2019 2 min read

WABUNGE kadha sasa wanataka maafisa wakuu wa Shirika la Feri Nchini (KFS) na Kikosi cha Kulinda Bahari (Kenya Coast Guard) kuwajibikia ajali iliyotokea katika kivuko cha Likoni ambapo mama na bintiye walifariki baada ya gari lao kuteleza na kutumbukia baharini.

Kwenye kikao na wanahabari Jumatano katika majengo ya Bunge, viongozi hao wapatao 11 walitaja vifo vya Bi Miriam Kigenda na bintiye Amanda Mutheu kama vya kusikitisha kwani vilitokea kutokana na kile wametaja ni utepetevu wa maaafisa wa mashirika hayo ya serikali.

Wakiongozwa na Mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko na mwenzake wa Lunga Lunga Bw Khatib Mwashetani viongozi hao 11 aliuliza mahala ambako waokoaji wa feri hiyo walikuwepo wakati wa tukio hilo.

“Maafisa wa KFS, KCG na hata jeshi la wanamaji sharti waadhibiwe kufuatia kisa hiki. Tunaamini kuwa kilitokea kutokana na utepetevu wa maafisa wa mashirika haya,” akasema Bi Mboko.

Akaongeza: “Ni aibu kwamba mpaka sasa (Jumatano) maafisa wakuu wa KFS hawajajitokeza na kuungama kuwa na Bi Kigenda na mtoto Amanda walipoteza maisha yao kutokana na kutomakinika kwao kazini.”

Wabunge wengine walioandamana na wawili hao (Mboko na Mwashetani) ni; Gladys Wanga (Homa Bay), William Kamoti (Rabai), Elsie Muhanda (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kakamega katika Bunge la Kitaifa), Ruweidha Obo Mohamed (Lamu), Teddy Mwambire (Ganze) na Beatrice Adahala (Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Vihiga).

Ajali

Wabunge hao walisema maafisa wakuu wa mashirika hayo wanapasa kuchunguzwa endapo uchunguzi utabaini kuwa kutowajibika kwao ndiko kulisababisha ajali hiyo na kusababisha vifo hivyo.

Wakati huo huo Mamlaka ya Shughuli za Majini (Kenya Maritime Authority) imeitaka pia imemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika la KFS Bakari Gowa kuwajibikia ajali hiyo.

Lawama kama hizo zilielekezwa kwa Bw Gowa na Mshirikishi wa Ukanda wa Pwani John Elungata.

“Feri yenyewe ni kuukuu na milango yake haingeweza kufungika. Usimamizi wa feri unapasa kuwajibikia kosa hilo ambalo lilihatarisha usalama wa abiria,” akasema.