Mkataba wa Ruto na Muturi wazimwa

Mkataba wa Ruto na Muturi wazimwa

NDUBI MOTURI Na CHARLES WASONGA

JOPO la kutatua mizozo ndani ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) limefutilia mbali mkataba wa kubuni muungano uliotiwa saini kati ya chama cha Democratic Party (DP) na muungano wa Kenya Kwanza (KKA) unaoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Katika uamuzi huo uliotolewa Ijumaa, jopo hilo liliamua kuwa mkataba huo ambao ulitiwa saini na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, kwa niaba ya chama cha DP, haukuidhinishwa na maafisa wa chama hicho.

“Mkataba huo wa muungano uliotiwa saini kwa niaba ya DP na Bw Muturi ulifanywa bila idhibiti ya chama cha DP na hivyo ni batili,” akasema mwenyekiti wa jopo hilo Jessica M’mbetsa.

Jopo hilo pia lilisema kuwa uteuzi wa Bw Muturi kama kiongozi wa DP haukufanywa kisheria kwa sababu hakuwa amedumu chamani kwa zaidi ya miezi sita, kulingana na hitaji la Katiba ya DP.

“Uteuzi wa mshtakiwa wa kwanza (Muturi) kuwa kiongozi wa chama cha Democratic Party na kongamano maalum la wajumbe (NDC) mnamo Februari 20, 2022 ulifanywa bila kufuata utaratibu uliowekwa kwenye katiba na hivyo ni batili,” akasema.

Uamuzi huo unafuatia malalamishi yaliyowasilishwa kwa jopo hilo na maafisa watatu wa chama cha DP.

Katika malalamishi hayo ya Aprili 11, Naibu Katibu Mkuu wa DP Wambugu Nyamu, Daniel Munene na Kingori Choto walipinga hatua ya Bw Muturi kutia saini mkataba wa muungano na Kenya Kwanza kwa niaba ya DP, wakisema hawakushauriwa.

Aidha, walisema kuwa Bw Muturi alijitwika cheo cha kiongozi wa chama hicho cha DP licha ya kuwepo kwa pingamizi kutoka kwa baadhi ya wanachama na maafisa wakuu.

“Mshtakiwa amekuwa akiendesha shughuli za chama kisiri na ameamua kuficha habari muhimu za chama bila sababu maalum. Kwa mfano, ameficha maamuzi ya NDC iliyofanyika Februari 20, 2022,” yakasema malalamishi hayo.

Bw Muturi alitia saini mkataba wa kujiunga na Kenya Kwanza katika hafla iliyofanyika katika mkahawa wa Hermosa, mtaani Karen, Nairobi, mnamo Aprili 9, 2022.

Wengine waliokuweko wakati wa kutiwa saini kwa mkataba huo walikuwa ni kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, miongoni mwa wandani wengine wa Dkt Ruto.

Naibu Rais alisema kutiwa saini kwa mkataba huo kulijiri baada ya msururu wa mazungumzo yaliyofanyika ndani ya wiki kadhaa kati ya Kenya Kwanza na uongozi wa DP.

“Ni furaha yangu kwamba leo (Aprili 9, 2022) tumeungana na chama chenye historia ndefu katika Jamhuri ya Kenya. Chama chenye alama za maendeleo nchini na ambacho kiliongozwa na rais mstaafu Mwai Kibaki,” Naibu Rais rais akasema.

Maafisa wa DP waliokuwepo wakati wa kutiwa saini kwa mkataba huo walikuwa ni mwenyekiti wa chama hicho Esau Kioni, Katibu Mkuu Jacob Haji na Mlezi Joseph Munyau.

  • Tags

You can share this post!

Timbe atwaa Kombe la FA Thailand

Tammy Abraham aweka rekodi mpya ya ufungaji wa mabao...

T L