HabariSiasa

Mkataba wa Uhuru na Ruto hautatumika na Jubilee kuteua mwaniaji wa urais 2022

January 10th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIRANJA wa wengi bungeni Benjamin Washiali (pichani kati) amesema kuwa chama cha Jubilee haitaheshimu mkataba wowote wa maelewano (MoU) wakati wa uteuzi wa mgombeaji wa urais wake katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Washiali alisema japo kuna madai kuwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto waliafikiana kuongoza kwa vipindi viwili vya miaka 10 kila mmoja “hayo yalikuwa ni makubaliano kati ya watu wawili”.

“Ikiwa Rais Kenyatta alikubaliana na naibu wake mnamo 2013 kwamba atamuunga mkono ili naye (Ruto) aweze kuongoza kwa miaka 10, walifanya hayo wakati Jubilee ilikuwa muungano wa vyama vya TNA na URP. Lakini baada ya Jubilee kuwa chama kimoja mnamo Septemba 2016 MOU hiyo sasa haitambuliwi,” akasema Mbunge huyo wa Mumias Mashariki kwenye kikao na wanahabari Alhamisi katika majengo ya bunge, Nairobi.

Kauli yake inalandana na yake aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe aliyepuuzilia mbali mkataba huo akisema, “ulikuwa wa watu wawili”.

Bw Washiali alisema chama hicho kitafanya uteuzi wa mgombea urais wake, wakati ukitimu na Bw Ruto atashiriki katika zoezi hilo pamoja wengine ambao watajitokeza.

“Lakini nina imani kuwa Naibu Rais ataibuka mshindi kwa sababu anaungwa mkono na wanachama wengi wa Jubilee kutokana na rekodi yake ya maendeleo,” akasema.

Mbunge huyo alisema mtindo wa mtu fulani kupendekezwa kwa kiti cha urais umepitwa na wakati katika siasa za taifa hilo na hata katika mataifa mengine ya ulimwenguni kwani hauwahi kuleta ufanisi wowote.

“Tunakumbuka kwamba Rais Kenyatta alipendekezewa na Rais mstaafu Moi mnamo 2002 na akaanguka… na mwaka jana Barack Obama akampekeza Bi Hillary Clinton lakini akashindwa na Donald Trump,” akasema.

Bw Washiali aliandamana na wabunge Emmanuel Wangwe (Navakholo), Mathias Robi (Kuria Magharibi), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Benard Shinali (Ikolomani).