Habari Mseto

Mkazi ashangaza wanakijiji kufukuza mkewe aishi na mume mwenzake

July 20th, 2020 1 min read

Na OSBORN MANYENGO

MWANAMUME katika Kaunti Ndogo ya Kiminini, Kaunti ya Trans-Nzoia ameshangaza wanakijiji kwa kumtimua mkewe wa muda mrefu na kuishi na mwanamume mwenzake chumba kimoja.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Millicent Ndeta, 50, alisema mumewe ambaye walizaa pamoja watoto kumi, aliamua kuishi na mwanamume huyo ambaye ni mkazi wa Mombasa.

Bi Ndeta alisema alimkaribisha mwanaumume huyo kwa boma lake baada ya mumewa kumjulisha kwamba ni mgeni wao.

Alisema baada ya siku chache, tabia ya mumewe ilianza kubadilika ambapo mgeni na mumewe waliamua kulala kwa chumba kimoja, huku yeye akipewe chumba tofauti na watoto wao pia wakipewa chumba kingine.

“Ni miaka miwili na miezi saba sasa tangu mume wangu abadilishe tabia yake akaniacha na kuishi na mwanaume mwenzake. Niliripoti kwa kituo cha polisi cha Bikeke lakini nikaambiwa bado maafisa wa polisi wanafanya uchunguzi wao” akasema.

Hata hivyo, Taifa Leo ilifanikiwa kumhoji mumewe, Bw Leonard Ndeta, 54, ambaye alikiri kuishi na mwanamume badala ya bibi yake lakini akasisitiza yeye si shoga.

Kulingana naye, aliamua kumleta mwanamume nyumbani ili iwe rahisi kumfurusha mkewe.

“Siwezi kwenda kinyume na maadili ya Mungu kwa kumwoa mwanamume mwenzangu. Mke wangu alikuwa kero kwangu na nilijaribu njia zote kumtaliki nikashindwa, ndipo nikamwalika rafiki yangu nyumbani kwangu ili mke wangu asipate nafasi kuwa karibu nami,” akaeleza.

Wawili hao wamejaliwa watoto kumi, lakini wawili walifariki na kusalia na wanane pamoja na wajukuu.

Imebainika maisha yao yalianza kwenda mrama mnamo 2016, wakati Bw Ndeta alitoka Mombasa mahali ambapo alikuwa akifanya kazi ya uendeshaji gari.

Kesi yao iko mbele ya maafisa wa usalama huku Bi Ndeta akitaka haki itendeke kwani kwa sasa hana pa kuishi.

Alisema biashara walizoanzisha pamoja zimedorora kwa sababu ya kutoelewana kwao, na amekosa mbinu nyingine ya kujitafutia riziki.