Habari Mseto

Mke ajigeuza umbo baada ya kunyofoa nyeti za mumewe

September 8th, 2018 2 min read

Na DIANA MUTHEU

Mwanamke aliyetoroka baada ya kudaiwa kunyofoa nyeti za mpenziwe na kummwagia asidi usoni eneo la Kinoo, Kaunti ya Kiambu alikamatwa Jumapili katika Kaunti ya Kwale akiwa amejibandika majina bandia.

Jane Wanjiku Wacuka alidaiwa kumvamia David Kyande wiki iliyopita na kutorokea Pwani.

Alipokamatwa, Wanjiku alipatikana na kitambulisho kipya akiwa amevalia buibui na kujifanya Mwislamu.

Ilifichuka kuwa Wanjiku alikimbilia Kwale na kujitambulisha kama Evelyne Wacuka Wangari na alikuwa anajaribu kuomba kazi katika baa ya Tandori eneo la Diani wakati alipokamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Makupa, Mombasa.

“Mwanaume huyo alikuwa mpenzi wa zamani wa Bi Wacuka na anaitwa Paul Kyande. Bi Wacuka alimualika wapate kinywaji katika baa moja ambapo alitia dawa za kulevya katika kinywaji chake,” afisa huyo alisema.

Afisa huyo aliongeza kuwa baada ya mwanaume kulala kutokana na uzito wa dawa ile ya kulevya, mshukiwa huyu alimpeleka katika nyumba yake.

Mwendo wa saa nane usiku huo, wanaume wawili waliingia ndani ya nyumba yake, wakammwagilia mwanaume huyo asidi kwenye macho na kumpora mali yake yote.

Kuongeza msumari moto kwenye donda, Bi Wacuka alimfanyia unyama mpenzi wake wa zamani kwa kuikata sehemu yake ya siri na kuitupa kwenye choo.

Bw Kyande anaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Kenyatta(KNH).

Mmoja wa washukiwa kwa majina, Joshua Ngugi alikamatwa Jumatano, huku polisi wakimsaka mwenzake aliye mbioni.

Kwa upande wake, Bi washuka aliyekamatwa katika Kaunti ya Kwale alikuwa amebadilisha majina, umri na pia dini yake.

“Tulipomkamata, alikuwa na kitambulisho bandia. Pia, alibadili dini yake na kuwa Mwislamu na alivalia buibui jeusi, ,” afisa huyo alisema.

Baada ya kukamatwa, mshukiwa huyu alipelekwa katika kituo cha polisi cha Makupa, Mombasa na hapo jana alisafirishwa hadi Nairobi kukabiliana na mashtaka.

Tulipokagua kitambulisho chake kipya, mshukiwa huyu alikuwa amebadilisha jina lake na kujitambulisha kama Margaret Njoki Ngigi, huku akidai kuwa alikuwa na miaka 30.

Afisa huyo alithibitisha kuwa baada ya tukio hilo, mshukiwa alisafiri kuelekea Mombasa usiku huo na akafika mjini Agosti 29. Alikodisha nyumba Mshomoroni na baada ya siku chache, akaanza kutafuta kazi Diani, Kwale katika hoteli moja.

“Amekuwa Ukunda kwa siku mbili, akabadilisha namba yake ya simu. Pia alimhadaa kimapenzi mvulana mmoja huko Diani na kutumia kitambulisho cha mpenzi huyo mpya ili kusajili kitambulisho bandia,” aliongeza.

Katika fomu ya kuomba kazi ambayo alikuwa amewasilisha katika hoteli ile, Bi Wacuka alieleza kuwa anaishi Likoni na amewahi kufanya kazi katika shule ya St Augastine Academy, ila hakueleza iko wapi.

Pia alisema amewahi kufanya kazi katika baa na hoteli mbalimbali huku Mombasa na pia Nairobi ikiwemo Lollipop,Scratch Bar and Lounge ,Fine Breeze Resort.

“Kwa sasa mimi nafanya kazi kama mhudumu katika baa ya Duos wines and spirit,”aliandika katika fomu hiyo.