Dondoo

Mke aliyeenda kuokoa ndoa kwa mganga alishwa talaka

February 7th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Kagumo, Kirinyaga

MWANADADA mmoja alijuta baada ya kupewa talaka na mumewe akidai alikuwa akimtembelea mganga kupata hirizi.

Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka saba na kujaliwa mtoto mmoja.

Yadaiwa mwanadada alishawishiwa na marafiki zake kutembelea mganga mmoja maarufu Kagumo, anayesemakana kutatua shida za ndoa.

Ingawa mume wake huwajibikia majukumu ya familia, mwanadada alitaka awe akimpa pesa zote anazolipwa.

Baada ya kumtembelea mganga kwa miezi kadhaa, hirizi haikuonekana kufanya kazi. Inasemekana polo aliendelea kukazia mfuko naye mwanadada hakuchoka kwenda kwa mganga.

Kulingana na mdokezi, mganga huyo ni mraibu wa pombe sawa na mume wa mwanadada. Majuzi, wawili hao walikutana katika baa moja, na baada ya kulewa, mganga alitoboa siri.

“Hata mke wako ni mteja wangu shupavu, hutembea kwangu kupata hirizi ya kunogesha mahaba kati yenu,” alisema mganga. Jamaa alionekana kushangazwa na habari hizo, lakini akatuliza ghadhabu zake. “Ndoa zina changamoto nyingi, wanawake hawakosi vituko,” alisema jombi.

Yasemekana kalameni alipofika kwake, alitaka mkewe kumueleza bayana sababu za kwenda kwa mganga. “Kila kitu unachofanya gizani ninakijua. Wewe na mganga mna uhusiano gani?” aliuliza. Boma hilo liliwaka moto, mwanadada alijitetea kwamba polo hamtoshelezi kimapenzi.

“Mume asiyetosheleza mke wake unatarajia apelekwe wapi?” alimjibu kwa madharau. Kwa ghadhabu jamaa aliagiza kidosho kuondoka mara moja akisema hangevumilia ndoa ya aina hiyo.

“Huyo mganga anayekuhudumia nenda kwake akuoe na kukutimizia mahitaji yako,” jamaa alisema. Kilio cha kipusa hakikubadilisha uamuzi wa polo kwani maji yalikuwa yamemwagika na hayangezoleka.