Makala

Mke aliyeua mumewe kwa kisu aepuka kifungo kirefu baada ya msamaha wa baba mkwe

Na TITUS OMINDE August 21st, 2024 2 min read

MWANAMKE aliyepatikana na hatia ya mauaji ya mume wake mnamo Jumanne alipewa hukumu ndogo baada ya kuomba msamaha kwa baba mkwe kutokana na kosa hilo.

Inadaiwa Abigael Yego mwenye umri wa miaka 32 alimuua marehemu wakati wa ugomvi wa kinyumbani pale alipomnyang’anya marehemu kisu cha mauti kabla ya kumdunga shingoni.

Abigael alipatikana na hatia ya kumdunga kisu Livingstone Kamau hadi kufa kwa kutumia kisu cha jikoni ambacho alidaiwa kumpokonya marehemu ambaye alimvamia katika nyumba yao ya ndoa usiku wa Juni 17, 2019 katika kituo cha biashara cha Moi’s Bridge, Kaunti ya Uasin. Gishu.

Akijitetea, aliambia mahakama kuwa haikuwa nia yake kumshambulia marehemu bali alikuwa akijitetea ila kwa hasira alimgeuzia kisu na kusababisha kifo chake wakati wa makabiliano hayo.

Baada ya miaka mitano ya mchakato wa kesi, Jaji Reuben Nyakundi wa Mahakama Kuu mjini Eldoret alimpata mshtakiwa na hatia ya mauaji kinyume na kifungu cha 203 kikisomwa na kifungu cha 204 cha kanuni za adhabu.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Nyakundi alisema upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo shaka kwamba Yego alimuua Kamau hivyo basi alistahili hukumu iliyoambatana na mashtaka kwa mujibu wa sheria.

Akijitetea kabla ya hukumu, mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa anajutia kitendo chake kilichosababisha kifo cha mumewe.

Kabla ya tukio, wawili hao walikuwa wamedumu katika ndoa kwa zaidi ya miaka mitano.

Awali, mahakama iliambiwa kuwa ndoa hiyo ilikumbwa na ugomvi wa kinyumbani wa mara kwa mara ambapo mshtakiwa alidai kuwa marehemu alikuwa akimtia majeraha aghalabu.

“Nimejuta sana kuchangia katika kifo cha mume wangu ambaye nilimdunga kisu wakati wa kujikinga dhidi ya uvamizi wake. Tayari nimefikia familia ya marehemu na kuiomba msamaha ambapo baba wa marehemu alikubali ombi langu,” Abigael aliambia mahakama.

Mahakama ilikiri kupokea barua kutoka kwa babake marehemu, Josphat Mwangi, ambaye alikubali ombi la msamaha wa Abigael.

Bw Mwangi ambaye alipewa nafasi na mahakama kueleza maoni yake kuhusu jambo hilo hilo alithibitishia mahakama kwamba mshtakiwa pamoja na familia yake waliomba msamaha na kama baba alimsamehe akibainisha kuwa hakuna hukumu itakayomrudisha mwanawe na kuwa Mkristo alilazimika kusamehe na kumwachia Mungu hukumu ya mwisho.

“Kama familia, tayari tumemsamehe mshtakiwa na tumeiachia mahakama uamuzi wake ambao tutaukubali,” Bw Mwangi.

Abigael ambaye alikuwa nje kwa bondi pia alipata afueni kutoka kwa maafisa wa watoto ambao waliambia mahakama kwamba mshtakiwa ambaye alikutana na rafiki mpya wakati kesi ikiendelea alikuwa akinyonyesha mtoto wa miezi minne ambaye alikuwa na matatizo ya kiafya na alistahili huduma maalum.

Ni bayana kwamba ripoti ya afisa wa watoto ilizingatiwa wakati wa kutoa hukumu.

“Kufuatia matukio kuhusiana na tukio hili na ushahidi uliotolewa katika mahakama hii, ninakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela,” akaamuru Jaji Nyakundi.