Habari Mseto

Mke amekiri mtoto wetu wa tatu si damu yangu, natamani ardhi ipasuke inimeze!

January 15th, 2024 1 min read

MUULIZE SHANGAZI:

Nimekuwa nikishuku kuwa mke wangu alitembea nje na kuzaa mtoto wetu wa tatu. Amekana kwa muda mrefu lakini hatimaye juzi aliungama nilipotishia kwenda hospitalini kuthibitisha. Nahisi vibaya kulea mtoto ambaye si wangu. Nishauri.

Mke wako ana makosa ya kwenda nje ya ndoa. Mtoto ni matokeo ya kitendo hicho, hana hatia. Kama uko tayari kumsamehe mke wako, mkubali pia mtoto huyo na umpende kama wako.

Mke ataniona kama zuzu nikimuuliza ushauri?

Nina mke na watoto wawili. Nimeajiriwa na mshahara wangu ni mzuri lakini pesa zangu nyingi huishia kwa mambo yasiyo muhimu. Mke wangu anajua mengi kuhusu uwekezaji lakini naona aibu kumuuliza.

Ukiona aibu kumshirikisha mke wako katika mipango ya kifamilia hamtawahi kuwa na maendeleo. Hakuna mtu anayejua kila kitu. Kama unataka mabadiliko kuhusu matumizi ya pesa zako, mshirikishe mke wako.

Anataka mali yetu yote iwe kwa jina lake

Mchumba wangu amenipa sharti la kumuoa. Kwamba tuandikishe mali yetu yote kwa jina lake ili kuthibitisha nampenda na sitawahi kumuacha. Waonaje?

Usikubali kufungwa macho na mapenzi. Mambo hubadilika. Yeye pia anaweza kukuacha na hiyo ina maana kwamba utaachwa bila chochote. Ni bora kuandikisha mali kwa majina yenu nyote ili kulinda maslahi ya kila mmoja wenu.

Mpenzi ataka nimuoe ila nahitaji muda zaidi

Mwanamke mpenzi wangu anataka tufunge ndoa mwaka huu. Tumekuwa pamoja kwa miaka minne na anasema muda huo unatosha kwa kila mmoja wetu kuamua kuhusu hatima ya uhusiano wetu. Nahitaji muda zaidi. Nifanyeje?

Mpenzi wako ana sababu nzuri ya kudai ndoa. Hata hivyo, ndoa kwa mwanamume huja na majukumu kwa hivyo anahitaji kujiandaa vyema. Ni vyema ushauriane naye kuhusu ambao unahitaji.