Kimataifa

Mke amhadaa mumewe ametekwa nyara kumbe ajivinjari na mpango wa kando!

June 11th, 2018 1 min read

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

MWANAMKE alimdanganya mume wake kwamba alitekwa nyara kumbe alikuwa akiponda raha na mwanamume mwingine hotelini.

Kulingana na polisi, Bi Margaret Namukose alimpigia simu mume wake Juni 7 na kumwambia alipanga kuhudhuria mkutano wa shule Kasangati, Wilaya ya Wakiso.

Mume wake aliingia wasiwasi wakati hakurudi nyumbani jioni na alipojaribu kumpigia simu, hakumpata.

Baadaye mume huyo alipokea simu kutoka kwa Margret ambaye alimwambia kuna wanaume waliomteka nyara, wakambaka na kumtupa msituni.

Mume wake alipiga ripoti kwa kituo cha polisi cha Kyebando na msako ukaanzishwa mara moja. Polisi walitumia teknolojia kutafuta simu yake ikabainika ilikuwa Kampala.

“Polisi walijitahidi sana kumtafuta mwanamke ambaye alidai alitekwa nyara na kubakwa, kisha ikapatikana alikuwa amedanganya ili waburudike wikendi na mpango wake wa kando,” akasema msemaji wa polisi wa Kampala, Luke Owoyesigire.

Mnamo Juni 8, mwendo was aa tano asubuhi, mwanamke huyo alitokea nyumbani na mume wake akampeleka katika kituo cha polisi. Aliambia polisi kwamba alijiokoa mwenyewe akaenda katika zahanati iliyokuwa karibu kufanyiwa uchunguzi wa matibabu.

“Polisi waliandamana na Margret hadi katika kliniki aliyotaja lakini hapakuwa na thibitisho lolote kwamba alipokea matibabu hapo.

Alipohojiwa zaidi, alikiri kwamba wakati wote ambapo polisi walikuwa wakimtafuta hakuwa ametekwa nyara bali alikuwa akijivinjari katika Hoteli ya Serena na mpenzi wake mpya,” akasema msemaji wa polisi.

Mwanamke huyo alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kira Road na alipangiwa kushtakiwa kwa kutoa habari za uongo.

-Imekusanywa na Valentine Obara