Habari Mseto

Mke anasafiri sana na kuniachia mtoto mchanga, nishauri

January 12th, 2024 1 min read

Kwako shangazi. Mke husafiri mara nyingi na mbali kikazi. Tuna mtoto mchanga na nahofia atakosa malezi ya mama yake. Nahisi pia hali hiyo ni hatari kwa maisha yetu ya ndoa. Nahitaji ushauri wako.

Kazi inaweza kuathiri vibaya maisha ya ndoa na familia. Watoto wanahitaji malezi na mapenzi ya wazazi. Mume na mke wanahitaji wakati wa kutosha pamoja. Shauriana na mke wako atafute kazi nyingine ama biashara.

Nampenda lakini siamini ananipenda kwa dhati

Mimi ni mwanamke wa miaka 31. Sijawahi kuwa na mpenzi. Kuna mwanamume anayenitaka kimapenzi. Nampenda lakini sina hakika iwapo ananipenda kwa dhati. Nitajuaje?

Unahitaji kuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwanza ndipo uweze kumfahamu vyema mwenzako na kujua iwapo anakupenda kwa dhati ama ana nia nyingine kwako. Kwa sasa kubali ombi lake.

Aliniacha nilipomwelezea rafiki yake ananinyemelea

Juzi nilimfahamisha mpenzi wangu kuhusu mwanamume rafiki yake aliyetaka tuwe na mpango wa kando lakini nikakataa. Sasa anatishia kuniacha akidai tunamcheza. Nifanyeje?

Ulikuwa na nia njema kumwambia mpenzi wako kuhusu rafiki yake. Lakini kwa kuwa ameonyesha hakuamini, itabidi uthibitishe. Mwambie mkutane naye ili amuulize kama kuna chochote kati yenu.

Mke wa mtu anayenipa pesa kila mara, juzi aliniambia ananipenda, nipe ushauri

Nina miaka 28 na ninaishi mjini nikitafuta kazi. Mwanamke jirani yangu amezoea kunipa pesa za matumizi akiniambia mimi ni kama nduguye mdogo. Juzi aliniita nyumbani wake akaniambia ananipenda. Ni mke wa mtu. Nifanyeje?

Mwanamke huyo ameamua kukunasa kwa vyovyote vile. Sasa umejua kuwa pesa anazokupa akikuita nduguye mdoyo ni mtego wa kimapenzi. Usikubali ombi lake kwa sababu mume wake akijua utakuwa hatarini.