Dondoo

Mke ashuku pasta ana mpango wa kando kwa kukataa wakiandamana harusini

June 12th, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

MACHAKOS

KIOJA kilishuhudiwa sehemu hii mke wa pasta alipomlaumu mume wake kwa kukataa kuandamana naye kwenda kuhudhuria harusi ya mwanadada muumini wa kanisa lake jijini.

Wawili hao walikuwa wamealikwa kuhudhuria harusi hiyo na awali walikubaliana kuandamana jijini siku ikifika.

“Pasta alikuwa amepanga kuandamana na mke wake lakini siku ilipofika alianza kumpiga chenga na kumpuuza ili asiandamane naye kuhudhuria harusi ya mwanadada huyo,”alisema mdokezi.

Siku ya kioja kelele ilisikika kutoka kwa pasta huku mke wake akimlaumu kwa kumruka katika mpango huo.

“Lazima niandamane na wewe upende usipende. Tuliahidiana vizuri kuwa tutaandamana pamoja kwenda kuhudhuria harusi lakini sasa unakataa. Liwe liwalo naandamana na wewe,” mke wa pasta alisema.

Hata hivyo pasta alimpuuza na kumtaka mke wake kubaki nyumbani ili aende akamwakilishe. “Itabidi ubaki papa hapa nyumbani.

Nitaenda kukuwakilisha kwa hivyo usiwe na wasiwasi. Baki hapa nyumbani ukilinda boma na watoto,” alisema pasta.

Hata hivyo mkewe alisisitiza kuwa angeandamana naye.

“Sibadilishi msimamo wangu hata kidogo. Lazima niandamane nawe la sivyo sisi sote tubaki hapa nyumbani,” mama alisema.

Mke wa pasta alikaa ngumu mpaka pasta akakata tamaa kwa kuwa mkewe alishikilia msimamo wake kabisa wa kutaka kuandamana naye.

Yasemekana ilibidi pasta kukatiza safari yake ya kuhudhuria arusi hiyo baada ya mkewe kukaa ngumu. Hata hivyo haikujulikana kiini cha pasta kutotaka kuandamana na mkewe kuhudhuria arusi hiyo.

Kulingana na mdokezi, mkewe pasta alishuku mumewe alikuwa na mpango tofauti jijini kando na kuhudhuria harusi.