Habari Mseto

Mke asimulia jinsi alitumiwa na wawazi wake kumfilisisha mumewe

January 29th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

MWANAMUME mmoja katika mahakama ya Nakuru amemfikisha mama mkwe wake kizimbani kwa kile alichotaja kuwa kugeuzwa kitega uchumi.

Akisimama mbele ya hakimu mkazi mkuu Daisy Mosse wa mahakama ya Nakuru, Eric Kinyanjui alisema mkewe Esther Nduta (pichani) alikuwa akimwibia simu, nguo na pesa na kuwapelekea wazazi wake waliokuwa wakimtuma.

Nduta aliyetumika kama shahidi dhidi ya mamake alisema tangu aolewe amekuwa akitekeleza wizi ili kudumisha uhusiano mwema na wazazi wake waliokuwa wakimtegemea awafanyie kila kitu.

Wakati mmoja Esther aliungama mbele ya korti kuwa aliwahi kuiba Sh14,000 kutoka kwa mumewe na kumpelekea mama yake.

Baadaye alijutia akaamua kuachana na uovu huo lakini wazazi wake hawakuchukulia jambo hilo vizuri wakaamua kulipiza kisasi.

Walimpokonya mtoto wake mmoja wa kiume na kumkatalia, ndipo mumewe Eric Kinyanjui akaamua kuwashtaki.

Eric Kinyanjui akisimama mbele ya mahakama ya Nakuru kumshataki mama mkwe kwa kujaribu kumfilisisha. Picha/Richard Maosi.

Esther alisema wazazi wake walifanya hivyo ili wapate msaada kutoka kwa majirani na marafiki.

“Ninawaheshimu kama wazazi wangu lakini sitakubali mniharibie ndoa, ninaomba mahakama inisaidie kurejesha mwanangu ,”alisema.

Kwa upande mwingine wazazi wa Nduta Bw Joseph Kinyua na Elizabeth Kinyua walipinga madai hayo wakisema walikuwa na uwezo wala hawakutegemea misaada.

Aidha waliongeza kuwa hawatambui ndoa kati ya binti yao na Bw Eric Kinyanjui, kwa sababu alikuwa ‘amemwiba’ binti yao bila kumlipia mahari.

“Eric ameshirikiana na binti yangu kuepuka lawama, hawajali maslahi ya watoto wao ndio sababu wametuachia mzigo wa kulea mtoto wao mmoja,” Joseph alisema.

Bi Kinyua alijitetea akisema binti yake alikuwa akizurura ndio maana aliamua kumchukua mjukuu wake amsaidie kulea.

Bi Elizabeth Kinyua akijitetea dhidi ya madai ya kukatalia mtoto wa binti yake katika mahakama ya Nakuru. Picha/Richard Maosi

Alisema binti yake alikuwa akimsingizia mbele ya korti na wala hakuwa na nia ya kumpokonya mtoto wake kama alivyokuwa akidai.

“Kuanzia leo mimi sio mama yako mzazi, nenda ukamtafute mwingine,” Bi Kinyanjui alisema.

Nduta na Eric waliomba mahakama iwasaidie kurejesha mtoto wao ambaye hakuwa katika hali nzuri ya afya.

Kulingana nao, mwanao alikuwa ameshambuliwa na viroboto na alihitaji kukaguliwa na daktari haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo, mahakama ilipuuza ombi lao hadi kesi itakapomalizika.

Kesi itaendelea hapo Februari 15.