Mke asukumia mume mhanyaji kipusa

Mke asukumia mume mhanyaji kipusa

Na MWANDISHI WETU

KIEMBENI, MOMBASA

KALAMENI wa hapa alijipata kwenye njia panda baada ya mkewe aliyemuoa takribani miaka mitano iliyopita kumlazimisha aoe mke wa pili badala ya kuendelea kuchepuka na wanawake wengine nje ya ndoa.

Inasemekana baada ya jamaa kuoa mwanamke huyo, hakuacha kunyemelea vipusa wa mtaani, jambo lililomkera mkewe sana.

Mke wa polo alishtua wengi alipotoa kauli iliyomshangaza mumewe.

“Usidhani sijui mambo unayoendeleza mtaani. Najua una mpango wa kando ndio maana huwa hautulii hapa nyumbani. Kama hautosheki na mimi nakusihi uoe mwanamke mwingine na sitakuwa na shida. Nitakubali kuwa na mkemwenza,” demu alimwambia jamaa.

Jamaa alizubaa lakini mkewe alishikilia msimamo wake kabisa.

“Haiwezekani. Umejuaje nina mpango wa kando? Siwezi kuoa mke wa pili,” polo alisema.

Hali ilizidi kuchacha demu alipodai kumwacha polo iwapo hangekubali kuoa mke wa pili.

“Unayechepuka naye huko nje namjua. Alikuwa rafiki yangu na ninamjua vizuri kukuliko. Heri umuoe kama unataka mambo yako yawe sawa. Sitaki uniletee magonjwa ya zinaa hapa kwa sababu ya uzinifu wako,” demu alisema.

Jamaa kwa upande wake aliwaza na kuwazua na kudai hakuwa na uwezo wa kuishi na wanawake wawili.

“Siwezi kuishi na wanawake wawili. Ni wewe unanitosha,” polo alisema.

“Kama huna uwezo wa kuishi na wanawake wawili unanipuuza kwa nini? Unashindana na nani huko nje kwa uzinifu? Fanya uamuzi wako haraka kabla sijachukua hatua,” demu alisema.

Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya polo kusukumwa na mkewe aoe mke wa pili ili asitishe tabia ya kuchepuka.

You can share this post!

Kiungo wa CF Montreal Wanyama hatimaye apata mtoto wa kwanza

NASAHA: Kufeli kunapaswa kukupa nguvu mpya badala ya...

T L