Habari Mseto

Mke ataka talaka kwa kunyimwa 'mlo wa usiku' na mumewe

May 6th, 2018 2 min read

Na BRIAN OCHARO

MWANAMKE mmoja amewasilisha kesi mahakamani kutaka apewe talaka ili kumaliza ndoa yake ya miaka 22 kwa madai kuwa mumewe amemnyima tendo la ndoa.

Lizzie Mapenzi Harrison anataka ndoa kati yake na mumewe John Musunza Muthengi kusambaratishwa kwa kusema ndoa hiyo haiwezi kuokolewa kutokana na uzinzi wa mumewe unaochangia amnyime ‘mlo wa usiku’.

Kupitia kwa wakili wake Michael Oloo, mwanamke huyo alisema mumewe ametelekeza familia yake na kuondoka nyumbani. Alisema pia kuwa mwanamume huyo alikuwa akimpiga sana mara kwa mara, hatua ambayo humlazimu kuondoka nyumbani kwenda kwa jirani.

“Mlalamishi anasema kuwa kwa sababu ya udanganyifu katika ndoa, dhuluma na kutelekezwa, na utengano wa mara kwa mara, hawezi kuendelea kukaa katika ndoa hiyo. Anaamini kuwa ndoa hiyo haiwezi kuokolewa,” alisema katika stakabadhi alizowasilisha mahakamani.

Walifanya harusi eneo la Jomvu Kuu, Mombasa mwaka 1996 na wana watoto wawili ambao ni watu wazima.

Bi Mapenzi alisema ndoa yao ilianza kutatizika mwaka wa 2007 alipogundua kuwa mumewe alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, ambaye pamoja walikuwa na mtoto.

Kutoka wakati huo, amekuwa mkali kwake, alieleza. Kutokana na uhusiano wa mapenzi nje ya ndoa na mtoto mwingine nje ya ndoa, alieleza kuwa ulileta matatizo katika ndoa yao. Mama huyo alielezea hofu yake kuhusiana na mali yao, ambayo iko kwa jina la mumewe.

“Mwaka wa 2013, mume wangu alininyima tendo la ndoa kwa kuhamia chumba tofauti. Kutokana na hilo, nilihisi kutokuwa na thamani yoyote,” alisema.

Kutoka wakati huo mpaka leo, wamekuwa wakiishi vyumba tofauti kwa sababu mumewe amekuwa na uadui mkubwa na kushiriki mapenzi nje ya ndoa.

Mwanamke huyo alisema juhudi za kuokoa ndoa yake kwa kukutana mara nyingi na wazazi zimekataa kuzaa matunda kwa sababu mwanamume huyo amekataa kuacha uzinzi.

Zaidi, alikataa kugawanya mali yao zaidi ya kukataa kuwatunza wanawe ikiwe ni pamoja na kuwalipia karo ya shule.

Alieleza mahakama kuwa maisha kwake yamekuwa magumu sana tangu mumewe alipoanza uhusiano mwingine.