Habari Mseto

Mke huota akitaja jina la mwanamume mwingine

January 5th, 2024 1 min read

Kwako shangazi. Ninashuku mke wangu anatembea nje. Nimemsikia mara kadhaa akiota na mwanamume fulani kwa kumtaja jina. Nimeamua kwamba sitamuuliza hadi nipate ushauri kutoka kwako.

Ndoto hutokana na shughuli au mawazo yetu. Ni lazima kuna kitu kinachoendelea kati ya mke wako na mwanamume anayeota naye. Chunguza mienendo yake na mawasiliano ya simu ili upate ushahidi.

Mpenzi aliniacha kwa mataa ila sasa ataka turudiane

Kwako shangazi. Mwanamke mpenzi wangu aliniacha miaka miwili tulipokuwa tukipanga ndoa. Nilimpenda sana na hatua yake hiyo iliniacha taabani. Juzi alinipigia simu akiomba turudiane. Nishauri.

Inawezekana kwamba mpenzi wako alidanganywa na mwanamume mwingine. Lakini amegundua wewe ndiye chaguo la moyo wake. Kama bado unampenda na hujapata mwingine mpe nafasi tena.

Mbona kinadada wananikimbia?

Mambo shangazi. Nimetafuta mchumba kwa miaka mitatu sasa lakini sijafaulu. Wanawake tunaopendana huniacha baada ya muda mfupi bila sababu. Nifanyeje?

Siamini wapenzi wako wamekuwa wakikuacha tu bila sababu. Huenda wanagundua kuwa hawakupendi ama wewe ndiye hujui kupenda. Kama hujui kupenda, itabidi ujifunze ndipo uweze kudumisha uhusiano.

Mke wa jirani anitamani!

Shangazi nisaidie. Mke wa jirani yangu ameniambia ananipenda na anataka tuwe na mpango wa kando. Mimi pia nina familia. Lakini ni mrembo sana na sijui kama nitaweza kujizuia. Nifanye nini?

Ni lazima mwanamke huyo ana matatizo katika ndoa yake. Ukiingia katika mtego wake utaharibu ndoa yako. Itabidi utafute namna ya kumuepuka.