Mke kizimbani kwa madai alimmwagia ‘mpango’ petroli

Mke kizimbani kwa madai alimmwagia ‘mpango’ petroli

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMKE aliyemmwagia mafuta ya petroli mtaalam wa lishe katika Gereza kuu la Kamiti na kutisha kumuua kwa kumteketeza kwa moto, Ijumaa alishtakiwa kwa kujaribu kutekeleza mauaji.

Upande wa mashtaka unadai Sheila Andati Okwomi (pichani) aliapa kumfundisha adabu Nancy Wanjiru Njeri kwa madai alikuwa amemnyang’anya mume.

Sheila alikanusha Aprili 8, 2021 kuwa alijaribu kumuua Nancy kwa kumtupia mafuta ya petroli ndani ya gereza kuu la Kamiti.

Alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu Bi Wendy Kagendo Michemi.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema, atatii masharti atakayowekewa na mahakama. Kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda hakupinga ombi hilo la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Hata hivyo, Bw Gikunda aliomba mahakama itilie maanani shtaka linalomkabili mshtakiwa; adhabu yake ni kifungo cha maisha.

“Shtaka linalomkabili mshtakiwa adhabu yake ni kifungo cha maisha akipatikana na hatia. Naomba korti imwachilie kwa masharti makali,” Bw Gikunda alieleza mahakama.

Bw Gikunda aliongeza kuomba mahakama imwamuru mshtakiwa asiwavuruge mashahidi kwa njia yoyote ile atakapopewa nakala walizoandika katika idara ya uchunguzi wa uhalifu sugu katika afisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI).

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh600,000 pesa taslimu.

Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 14, 2021 kwa maagizo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

UDA yaondoa mamlakani maafisa walioteuliwa majuzi

Jinsi wanawake warembo wanavyotumiwa kuwapora madereva wa...

T L