Habari Mseto

Mke mchuuzi aililia serikali baada ya askari kumvua nguo

December 10th, 2018 1 min read

 

Gavana wa Kaunti ya Garissa Ali Korane katika kikao cha awali jijini Nairobi. Picha/Maktaba

Na ABDIMALIK HAJIR

MWANAMKE anayeuza miraa na chakula mjini Garissa, Jumapili alidai kwamba askari wa serikali ya kaunti hiyo walimvua nguo akabaki uchi kabla ya kumpeleka kituo cha polisi.

Bi Dowlay Duale Keinan alidai kwamba alifedheheshwa mbele ya umma na maafisa hao anaolaumu kwa kurarua mavazi yake ikiwa ni pamoja na hijabu na diraa, vazi refu linalovaliwa eneo hilo.

Mkuu wa polisi eneo la Garissa (OCPD) Aron Moriase alithibitisha kisa hicho na kusema kuwa uchunguzi unaendelea lakini ripoti za mwanzo zilionyesha kuwa mwanamke huyo alivua mavazi yake mwenyewe.

“Tunaendelea kuchunguza suala hilo ingawa tulielezwa kwamba aliwachochea wanawake wengine dhidi ya maafisa hao, tutapata ripoti kamili kuhusu kisa hiki Jumanne,” aliambia Taifa Leo kwa simu.

Mwanamke huyo alidai kwamba maafisa hao walimwambia yeye na wafanyabiashara wengine waandamane nao hadi ofisi zao kwa kuuzia bidhaa eneo lisiloruhusiwa.

“Tulipoenda katika ofisi zao hakukuwa na yeyote na wakadai wao ndio walikuwa kazini na ni wakati huo waliporarua mavazi yangu nikabaki na chupi pekee,” alisema.

“Nikiwa nusu uchi hivyo, walimuita polisi wa utawala mwanamke ambaye alinifunga pingu kisha wakanitupa katika gari lao na kunipeleka kituo cha polisi kilichoko mita chache kutoka ofisi zao,” alisema Bi Keinan.

Alidai kwamba maafisa wa polisi walimpitishia barabara yenye shughuli nyingi ya Kismayu hadi kituo cha polisi huku kila mtu mjini akimtazama akiwa uchi akafedheheka sana.

Serikali ya Kaunti imekuwa ikiwaondoa wafanyabiashara katika barabara za mji wa Garissa. Mwanamke huyo anayeuzia miraa katika kituo cha mabasi alisema hata maafisa wa polisi walishangaa na kuwaambia askari wa kaunti kumrejesha akavae.

Bi Keinan alimtaka Gavana Ali Korane na viongozi wengine kuhakikisha kuwa amepata haki akisema huwa anauza bidhaa sokoni ili kutafuta riziki.

“Ninamuomba gavana binafsi kuchunguza watu ambao ameajiri kama askari wa serikali yake kwa sababu hawajali na hawana utu,” alisema.