Dondoo

Mke mhanyaji ataka wahame usiku

January 13th, 2020 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KANGEMI, NAIROBI

Kioja kilizuka kwenye ploti moja mtaani humu baada ya mwanadada kumshurutisha jamaa kuhama ploti alipotishiwa maisha na mke wa landilodi kwa kumnyemelea mumewe.

Inadaiwa kwamba jamaa hakufurahishwa na shinikizo la mkewe na akashuku alitaka kukwepa jambo fulani.

“Mimi nimechoshwa na maisha ya huku. Hebu tuhame haraka. Tusimweleze yeyote tutakohamia na pia tutahama usiku,” kipusa alimueleza jamaa

Maneno haya yalimshtua polo zaidi. “Mwezi ulipoanza hukuniambia lolote kuhusiana na kuhama. Tena mbona tuhame usiku,” jamaa alimuuliza kipusa. Duru zinasema mwanadada alitishia kumuacha jamaa asipokubali kuhama.

“Kama hutaki kusikia ninachosema basi mimi nitakuacha hapa. Ishi peke yako. Sitakubembeleza,” mwanadada alitishia.

Jamaa alionekana kukerwa na maneno ya mkewe. “Hujaniambia sababu ya kutaka kuhama ghafla. Sitaki kusikia tena huo upuzi wako,” alimkaripia mkewe.

Inadaiwa mwanadada alipandwa na hamaki na kuanza kumfokea polo.

“Kama unataka nikueleze sababu ya kutaka kuhama utangoja milele. Ni wewe unakaa mbumbumbu. Elewa haraka,” kipusa alimfokea polo. Penyenye zinasema kipusa alitaka kuhama ploti baada ya kutishiwa maisha na mke wa landilodi.

Inadaiwa mke wa landilodi alikuwa amempata akila fuska na mumewe na akaapa kumuadhibu na kumuaibisha kwa wapangaji wenzake.

Hata hivyo, hakumfichulia mumewe sababu ya kumtaka wahame.

Duru zinasema kipusa aliamua kuondoka na kumuacha jamaa plotini.

“Kuna uwezekano unahepa jambo fulani. Kama si hivyo basi umeanza kutumia bangi. Sitakubali kubebwa kama mtu mjinga,” jamaa alimfokea kipusa.

Mwanadada alipoondoka ndipo jamaa alifahamishwa na wambea kilichotendeka naye akampigia simu kumfahamishwa kwamba alifanya vizuri kuondoka ili asiendelee kumuaibisha plotini.