Habari Mseto

Mke wa Cohen alaumu DCI baada ya mwili kupatikana

September 15th, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

MAUAJI ya kushtusha ya bwanyenye Tob Cohen yanayozingirwa na utata yameibua hisia kali huku mkewe, Sarah Wairimu Cohen, sasa akishutumu Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kwa kupanga njama ya mauaji hayo.

Akizungumza Ijumaa kupitia wakili wake Dkt Philip Murgor,  Bi Wairimu alimwelekezea kidole cha lawama mkurugenzi wa DCI, George Kinoti, huku akishuku alivyojua ulipokuwa mwili wa bilionea huyo.

“Bw Kinoti alijua hata kabla ya mwili huo kutolewa kwamba ulikuwa wa Tob Cohen, pengine mnaweza kumuuliza jinsi alivyofahamu. Wairimu hakuwa nyumbani kwa siku 17 zilizopita na eneo hilo limekuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi,” alisema Bw Murgor.

Kulingana na wakili huyo maarufu, wapelelezi walichukua funguo kutoka kwa wafanyakazi katika boma hilo na kuwaamrisha kutotoka nje, jambo walilotii.

Bw Murgor alifichua kuwa kulikuwa na mfereji wa majitaka uliowekwa upya simiti ili kuziba shimo ambalo polisi walichimba moja kwa moja.

“Kuna shimo la majitaka na lilikuwa limezibwa kwa simiti upya. Wote walijua ni hapo walitaka kuchimba, walichimba na kuondoa sehemu ya juu,” alisema.

Huku akisisitiza kuwa mteja wake, Wairimu, atasalia kuwa bila hatia hadi itakavyothibitishwa vinginevyo, alihoji ni vipi vyombo vya habari na wengineo walivypodai tajiri huyo alikuwa amefariki.

Mwili wa mwendazake ulitolewa ndani ya tangi ukiwa na majeraha mabaya nyumbani mwake Kitisuru, Nairobi, mnamo Ijumaa.