Dondoo

Mke wa kudharau mume aonywa vikali

August 21st, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

KATHERI, MERU

MAMA wa hapa alipata aibu ya mwaka alipozimwa na wazee kwa kujaribu kujifanya kiongozi wa familia na kumdharau mume wake hadharani bila haya.

Kwenye sherehe ya kufurahia mwana wao aliyehitimu chuoni iliyohudhuriwa na watu wa familia na marafiki, mama huyo alijitwika jukumu la mwenye boma na kumyamazisha mumewe kila alipojaribu kuzungumza akidai alikuwa amebobea kutoa hotuba na kusema angewakilisha mzee wake.

Kulingana na mdokezi, ukweli wa mambo ni kuwa mama alianza kukanyagia mzee chini baada ya kupandishwa cheo kazini na akazidi mumewe alipokosa kazi baada ya muda wa kandarasi kumalizika.

Hapo ndipo alianza kujigamba na kudai alisomesha watoto wake na kumtaka mume kumuunga mkono kwa kila jambo.

Siku ya sherehe baada ya watu kufahamiana, mama alichukua fursa ya kumpongeza mwanawe na kisha akaanza kueleza ratiba, kazi iliyofaa kutekelezwa na mzee wake.

Baada ya wazee kushindwa kustahimili tabia yake mmoja wao alisimama kidete na kumkatiza kwa kumpokonya kipaza sauti.

“Huoni unakiuka mila kuhutubia watu na mume wako bado yu hai? Kama umekuwa ukimdhalilisha hapa hatutakubali hilo litokee tukishuhudia. Fyata ulimi na utulie kama akina mama wenzako,” mzee aliamuru.

Juhudi za mama za kujaribu kujitetea ziligonga mwamba kwani watu walimzima na kumtaka kuwa mpole.

Mama alitulia kama maji ya mtungi na mzee akachukua jukumu la kuendeleza sherehe hadi tamati. Hakuna aliyejua kilichotokea baadaye kwa sababu mama alikosa kuwaaga wageni na kuingia chumbani baada ya sherehe akiwa amenuna kama andazi.