Habari Mseto

Mke wa pili kumzika mume aliyefariki Februari

December 22nd, 2019 1 min read

Na ANGELINE OCHIENG’

MJANE mmoja amepoteza haki ya kumzika mumewe wa ndoa baada ya Mahakama ya Kisumu wiki iliyopita kutoa amri mwendazake azikwe kwenye boma la mke wake wa pili.

Bi Siprosa Awino ambaye mumewe aliaga dunia miezi 11 iliyopita, aliwasilisha rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Kisumu akipinga uamuzi wa Hakimu Mkuu Mkazi Winfred Onkunya uliotolewa mwezi Juni wa kumruhusu mkemwenza Grace Were amzike mume wao marehemu Silivanus Nyang’wara Mwanja.

Bi Awino alidai kortini kwamba uamuzi huo haukufaa ikizingatiwa kwamba mashahidi wote walikuwa wamesema mwendazake azikwe kwake mtaani Nyalenda, Kisumu.

Kupitia wakili wake Bi Awino, haikuwa imebainika iwapo marehemu alikuwa na nyumba Kaunti ya Bungoma kulingana na mila na tamaduni za jamii ya Waluo jinsi ilivyokuwa ikidaiwa na mkewe wa pili.

Hata hivyo, Jaji Fred Ochieng’ alikataa ombi lake, akisema uamuzi na korti ya hakimu ilifaa kisha akatoa amri Bi Were aendelee na mazishi ya mumewe.

“Naunga mkono uamuzi uliokuwa umetolewa na korti ya hakimu kwa kuwa uliambatana na ushahidi uliotolewa. Rufaa hii imefeli kwa hivyo imepuuziliwa mbali,” akasema Jaji Ochieng’.

Jaji huyo pia alisema mapenzi na matamanio ya marehemu yanafaa kutimizwa huku akishikilia kwamba alikuwa na maboma mawili; Nyalenda na Bungoma na aliyajenga kwa kutimiza mila ya Waluo ya kubeba shoka, jembe na panga wakati wa kuweka msingi wa nyumba hizo.

“Uamuzi wa marehemu wa kuzikwa nyumbani kwake Bungoma si kinyume cha sheria za Kenya au tamaduni za Waluo,” akaongeza. Mwili wa marehemu Bw Nyang’wara umekuwa ukihifadhiwa kwenye mochari ya hospitali Life Care mjini Bungoma tangu kifo chake Februari 2, 2019.

Wakati wa mauti yake, alikuwa amekosana na Bi Awino na hawakuwa wameishi pamoja kwa muda wa miaka 28.