Habari Mseto

Mke wa Rais na wa Naibu waongezewa donge

May 25th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

HUKU Wakenya wakizidi kuteseka kutokana na ugumu wa maisha, afisi ya mke wa Rais Uhuru Kenyatta, Margaret Kenyatta na wa Naibu Rais William Ruto zimetengewa Sh723.6 milioni kwenye bajeti ya mwaka 2019.

Kiasi hicho ni mara tatu zaidi ya fedha ambazo afisi za Bi Margaret Kenyatta na Bi Rachael Ruto walitengewa mnamo 2013.

Fedha hizo zitaanza kutumiwa kwenye mwaka wa matumizi ya pesa za serikali wa 2019/2020 utakaoanza mnamo Julai.

Kulingana na taarifa ya makadirio ya fedha za serikali kutoka kwa Hazina ya Kitaifa, kiasi kikubwa cha fedha hizo kitatumika kulipia mishahara ya wafanyakazi, kugharimia usafiri na burudani.

Wawili hao walipokea Sh187.3 milioni mnamo 2013. Bajeti ya afisi ya Bi Kenyatta imeongezeka kutoka Sh114.4 milioni hadi Sh426.1 milioni, huku ya Bi Ruto ikiongezeka kutoka Sh72.9 milioni hadi Sh297 milioni.

Ongezeko hilo linajiri huku Rais Kenyatta akizidi kutoa miito kwa idara mbalimbali za serikali kupunguza matumizi ya fedha katika masuala yasiyo muhimu kama vyakula na safari.

Agizo

Serikali ilitoa maagizo kuwazuia maafisa wake wakuu dhidi ya kusafiri nje ya nchi bila ruhusa maalum kutoka kwa Rais. Serikali pia imekuwa ikifuatilia sana safari za maeneo mbalimbali humu nchini.

Haya yanajiri huku Wakenya wakiendelea kulalamikia ugumu wa maisha.

Wadadisi wa masuala ya kiuchumi pia wamekuwa wakilalamikia mtindo wa serikali kuchukua mikopo kutoka nchi za nje, hasa Uchina, wakionya kuwa ni mojawapo ya sababu ambazo zimemwongezea mwanamchi mzigo.

“Ni lazima serikali itathmini mfumo wake wa ufadhili wa bajeti ya taifa, kwani kuendelea kukopa madeni kutoka nje ni mwelekeo hatari ambao utazidi kumzidishia mlipaushuru mzigo zaidi,” asema Kwame Owino, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi Kuhusu Masuala ya Kiuchumi (IEA).