Kimataifa

Mke wa Rais wa Burundi alazwa katika hospitali nchini Kenya

May 29th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MKE wa Rais wa Burundi anayeondoka Pierre Nkurunziza amelazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi alikopelekwa kwa ndege baada ya kuugua.

Vyombo vya habari nchi Burundi vimeripoti kuwa Denise Bucumi Nkurunziza alisafirishwa kwa ndege ya shirika la Amref hadi Nairobi kwa matibabu ya dharura.

Burundi ni mojawapo ya nchi za Afrika zinazopigwa darubini kwa kutofuata maagizo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Aprili 2020 serikali ya nchi hiyo ilimfukuza mwakilishi wa WHO kwa kutilia shaka uwezo wa nchi hiyo wa kupima na kuzuia maambukizi ya corona.

Duru zinasema kwamba Denise alifika Nairobi akiandamana na wasaidizi wake. Kuwasili kwake nchini ni kitendawili kwa sababu serikali ya Kenya imepiga marufuku safari zote za ndege nchini.

Nkurunziza amelaumiwa kwa kupuuza vita dhidi ya corona na aliruhusu nchi hiyo kufanya uchaguzi wa urais ambao hakutetea kiti chake mwezi huu wa Mei.dE