Shangazi Akujibu

Mke wangu amezidi, anagawa asali kiholela plotini, nawazia kumtema

May 30th, 2024 1 min read

Mke wangu ana tabia ya kugawa asali kiholela. Katika ploti tunamoishi kuna vijana wanaoishi hapo na nasikia kwamba tayari amewagawia tunda. Nawazia kumtema. Nishauri

Bila shaka hiyo ni tabia mbaya lakini swali langu ni je una uhakika kuhusu uvumi huu. Fanya uchunguzi kamili kabla ya kumshutumu na ukipata ushahidi unaweza kufanya uamuzi wako.

Tamaa ya vimada afisini imezidi baada ya kupata madaraka, nisaidie

Tangu tuoane na mume wangu, nimekuwa nikivumilia tabia yake ya usherati ya kuwatongoza wanawake kazini mwao. Hali hii imezidi majuzi baada ya kupandishwa madaraka. Nifanyeje?

Una ushaidi upi kuhusu madai haya? Ikiwa hauna ushahidi basi koma kumharibia mumeo jina. Ikiwa una ushahidi wa kutosha basi sharti umchukulie hatua ifaayo ili usije ukaletewa magonjwa ya zinaa.

Nimeolewa ila wa kando anataka niwe mke wa pili

Nimeolewa kwa miaka minane sasa na pamoja na mume wangu tumejaliwa watoto wawili. Kwa miezi kadhaa sasa nimekuwa na uhusiano wa pembeni na mwanamume huyu ambaye anasema anioe awe mume wa pili. Naomba ushauri.

Hayo ni mageni kwangu kwa kuwa huu ni uhusiano ambao si wa halali. Pili, kuna hatari ya kupoteza ndoa yako kwa sababu mtu uliyekutana naye miezi michache iliyopita huwezi kumwamini.

Mke wa miaka 10 ataka kuniacha, najihisi vibaya kiasi cha kujitia kitanzi

Mke wangu wa miaka kumi anataka kuniacha na kumwendea mwanamume mwingine mwenye pesa. Tumejaliwa watoto wanne lakini hajali. Nimekuwa na mawazo ya kutaka kujiua. Nisaidie

Unakumbwa na msongo wa mawazo na hivyo unahitaji ushauri nasaha wa dharura. Pili, usiruhusu matendo ya mwenzio yakuathiri hivi. Ikiwa hakutaki na umefanya kila uwezalo kuokoa ndoa yako basi hauna budi ila kukubali na kuendelea na maisha. Kujiua si sululuhisho na watoto wako bado wanakupenda zaidi na kukutegemea.