Michezo

MKEKANI TENA: Huenda Neymar akose Copa America

June 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

BRASILIA, Brazil

NYOTA Neymar, ambaye anakabiliwa na madai ya ubakaji, alirejea mkekani baada ya kuumia kifundo cha mguu Jumatano timu yake ya Brazil ilipobwaga Qatar 2-0 katika mechi ya kirafiki kabla ya soka ya Copa America.

Neymar alionekana akifunika uso wake kwa mikono akiketi kwenye benchi baada ya kuchechemea kutoka uwanjani Mane Garrincha dakika 20 pekee ndani ya mechi hiyo.

Mfuko wa barafu ulifungwa katika sehemu ya chini ya mguu wa mshambuliaji huyu wa Paris Saint-Germain, huku maafisa wawili kutoka benchi la kiufundi wa Brazil wakimbeba kutoka uwanjani.

Jeraha hili lilipatikana siku tisa kabla ya Copa America kuanza nchini Brazil.

Dakika chache baada ya mvamizi matata wa Everton Richarlison kufungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 17, Neymar, 27, aliondoka uwanjani na maumivu katika kifundo chake cha mguu wa kulia.

Mshambuliaji wa Manchester City Gabriel Jesus alipachika bao la pili katika dakika ya 23, lakini macho yote yalielekezwa kwa Neymar, ambaye Shirikisho la Soka nchini Brazil (CBF) lilikuwa limesema amepata jeraha ndogo kabla ya uchunguzi hospitalini kudhihirisha hapo jana lilikuwa baya.

Jeraha baya kwa Neymar ni pigo kubwa kwa Brazil inayolenga kutwaa ubingwa wa Amerika Kusini kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2007.

Mapema Jumatano, rais wa CBF Rogerio Caboclo alikuwa amesisitiza kwamba Neymar atashiriki Copa America licha ya madai ya ubakaji, siku moja tu baada ya afisa mmoja wa ngazi ya juu katika shirikisho hilo kusema alikuwa tayari ‘kubashiri’ kwamba nyota huyu atajiondoa kikosini.

Licha ya uchunguzi wa polisi kuhusu madai hayo ya ubakaji na kuchapishwa kwa picha za kisa hicho kwenye mitandao ya kijamii, Neymar aliendelea kufanya mazoezi na wachezaji wenza kujiweka tayari kwa kipute cha Copa America kitakachoanza Juni 14.

Kabla ya mechi dhidi ya Qatar, Caboclo aliambia wanahabari kwamba mchezaji huyo ghali duniani atashiriki mashindano haya, mara ya pili katika kipindi cha wiki alitoa hakikisho hilo.

Akili

Matamshi yake yalijiri baada ya naibu wake Francisco Noveletto kunukuliwa nchini Brazil akisema kwamba alikuwa tayari ‘kubashiri’ kwamba Neymar hatashiriki Copa America.

“Hayuko tayari kiakili kushiriki Copa America na kuonekana na wanahabari,” alisema Noveletto.

Caboclo alijibu kwamba Noveletto hakuwa akizungumza kwa niaba ya CBF, tovuti ya Globoesporte.com ilisema.

Saa chache kabla ya kukutana na Qatar, Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro alisema anaamini Neymar, ambaye amepinga madai hayo ya ubakaji.

“Anapitia wakati mgumu wakati huu, lakini namwamini,” alisema Bolsonaro.

Katika kikao na wanahabari Jumatatu, kocha Tite aliulizwa maswali mengi kuhusu kisa hicho na athari yake kikosini. Akijaribu kukwepa suala hilo, Tite alisema “hatamhukumu” Neymar, ambaye alimtaja kama tegemeo, lakini akaongeza kwamba haimaanishi nafasi yake haiwezi kujazwa.

Sakata ya ubakaji ni kilele cha msimu mbaya Neymar amekuwa nao, uwanjani na nje ya uwanja.

Amesumbuliwa na jeraha, alipigwa marufuku mechi mbili kwa kutusi refa na kupiga shabiki mmoja, na kupokonywa unahodha wa timu ya Brazil. Aliteremka uwanjani saa chache baada ya mwanamke Najila Trindade Mendes de Souza aliyedai Neymar alimbaka kusimulia kisa hicho.

Runinga ya SBT ilihoji mwanamke huyo mwanamitindo, ambaye alikiri kupenda Neymar mwanzoni kabla ya kukerwa na tabia yake alipokutana naye katika hoteli moja jijini Paris nchini Ufaransa baada ya nyota huyo kumlipia nauli ya ndege na chumba katika hoteli hiyo.

Mapema juma hili, mamake Neymar, Nadine Goncalves alimtaka amsamehe Trindade na amrudie Yesu Kristo.