Habari Mseto

Mkemwenza auawa akienda kuoga

May 12th, 2019 1 min read

Na GERALD BWISA

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 22 mnamo Jumamosi aliaga dunia baada ya kudaiwa kudungwa kisu shingoni na mkemwenza katika kjiji cha Lukhuna, Kaunti ya Trans Nzoia.

Marehemu kwa jina Nancy Odima alikuwa ameenda kuoga bafuni saa tatu usiku na kumwacha mumewe na mwanao wa miezi saba, alipovamiwa na mkemwenza.

Kamanda wa Polisi wa Trans Nzoia Ayub Ali alieleza Taifa Leo kwamba wanashuku marehemu aliandamwa na mvamzi alipokuwa akienda kuoga.

“Tunashuku kwamba baada ya kukatwa shingoni kwa kifaa kilichonolewa kikanoleka, alijaribu kuelekea katika nyumba yake lakini akaanguka na kutokwa na damu nyingi hadi akafariki,” akasema Bw Ali.

Polisi waliofika kwenye eneo la tukio walipata marehemu amechinjwa na mwili wake ukageuzwa na kuangalia chini.

Polisi hao waliwakamata mume wa marehemu pamoja na mkewe baada ya kuokolewa mikononi mwa raia waliokuwa wakitaka kulipiza kisasi kwa kuwaua.

Hata hivyo, silaha iliyotumika kwenye maangamizi hayo haikupatikana katika eneo la tukio huku polisi wakiendelea na uchunguzi.

Mwili wa mwendazake ulipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitale.