Habari za Kitaifa

Mkenya aambia korti ni mke wa mlalamishi kutoka Nigeria

May 29th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA anayedaiwa kutumia jina la kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kumtapeli mwekezaji kutoka Nigeria Jude Olabwayo Veracruz takriban Sh25 milioni, Jumanne alifichua kortini kwamba mlalamishi ni mume wake.

Ufichuzi huu uliduwaza kiongozi wa mashtaka Naomi Wanjiru na kumfanya afyate ulimi.

“Mlalamishi katika kesi hii ni mume wangu. Hakuna ulaghai hapa. Mume humpa mke pesa za kugharimia mahitaji mbalimbali na hata kupiga jeki biashara. Wizi umetoka wapi? Hili ni suala la kinyumbani,” Bi Faith Mwikali Ndiwa alitoboa siri kortini.

Mwikali anayeshtakiwa kumlaghai Veracruz Sh25 milioni, aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “siwezi nikatoroka nchi yangu hata. Niende wapi?”

Mshtakiwa huyo alieleza mahakama kupitia mawakili wake watatu kwamba polisi wameipotosha mahakama wakidai hajulikani anakoishi jijini Nairobi ilhali wanajua anakoishi Veracruz mume wake.

Mshtakiwa huyo alimweleza hakimu mkazi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi kwamba dhamana ni haki ya kila mshtakiwa na hapaswi kuzuiliwa gerezani kwa sababu hafifu.

Alimsihi hakimu atumie mamlaka yake na kumwachilia.

Lakini Bi Wanjiru alipinga ombi hilo la dhamana akisema mshtakiwa amewakwepa polisi tangu mwaka 2022.

Hakimu alielezwa ilibidi polisi wawatumie marafiki wa karibu wa mshtakiwa kumfikia na ndipo wakamtia nguvuni.

Mahakama ilielezwa pasipoti ya mshtakiwa imeonyesha kwamba amesafiri mara nyingi nje ya nchi.

Lakini mshtakiwa alimjibu afisa wa polisi Konstebo Okoth anayechunguza kesi hiyo akisema “wananchi wa Kenya wanaruhusiwa kisheria kumiliki pasipoti.”

Mwikali alifikishwa kortini Jumatatu akikabiliwa na shtaka la kumtapeli Veracruz Sh25 milioni katika kashfa ya kuuzia Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa Nchini (Kemsa) neti zilizotibiwa.

Mwikali anadaiwa alimwonyesha Veracruz kandarasi ya kuuzia Kemsa neti zilizotibiwa za kuua mbu katika vita dhidi ya malaria.

Kandarasi hizo zilikuwa zimepewa kampuni zake mbili Ashley Dylan Limited na Faizel Limited.

Bi Wanjiru aliambia mahakama kwamba Mwikali alimweleza Veracuz kampuni zake Ashley Dylan na Faizel zilikuwa zimeshinda zabuni nambari IFT NO GF ATM MAL NFM-19/20-OIT-004 ya kuuzia Kemsa neti zilizotibiwa za kuua mbu za kudumu muda mrefu-(LLINs).

Bi Wanjiru aliongeza kusema Veracruz alieleza polisi mshtakiwa alimweleza kandarasi hii ilikuwa imekabidhiwa mkwewe Bw Odinga na kwamba amepungukiwa na fedha.

Mkwewe huyo Bw Odinga, ilidaiwa, alikuwa anahitaji msaada ndipo Mwikali akamrai Veracruz atoboke pesa za kukamilisha zabuni hiyo kisha apate faida kubwa.

Veracruz alimpa Mwilkali Sh25 milioni ndipo hatimaye akagudua ametapeliwa.

Mwikali alikana mashtaka manane ya kumtapeli Veracruz kati ya Juni na Desemba 2022 katika Kaunti ya Nairobi.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana lakini Bi Wanjiru akapinga akisema afisa wa polisi Bi Eunice Njue anayechunguza kesi hiyo pamoja na polisi wengine, “wanahitaji muda kuwasilisha hati ya kiapo kuelezea sababu za kupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.”

Hakimu mkuu aliamuru Mwikali azuiliwe katika gereza la Lang’ata hadi Jumatano (leo) atakaporudishwa kortini kuelezewa ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.

Bw Ekhubi aliamuru idara ya urekebishaji tabia iwasilishe ripoti kumhusu Mwikali kabla ya kuamua iwapo ataachiliwa kwa dhamana au la.