Habari Mseto

Mkenya amtaka kasisi Mwitaliano anayedaiwa kumzaa, kumtambua

October 10th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MWANAMUME Mkenya mwenye umri wa miaka 30 amegonga vichwa vya habari kimataifa kufuatia juhudi zake za kumsaka babake mzazi ambapo anayedai ni kasisi wa Katoliki Mwiitaliano aliyempachika mimba mamake akiwa na umri wa miaka 16.

Gerald Erobon ambaye amepania kujua ukweli, ameshinikiza Vatikan kuanzisha uchunguzi katika kisa hicho ambacho kimeangazia Kanisa la Katoliki na uozo unaoendelezwa na baadhi ya makasisi ikiwemo kushiriki ngono na watoto katika jamii iliyogubikwa na usiri.

Kulingana na ripoti, mamake Erobon, Sabina Losirkale aliyekuwa kijana chipukizi, alitungwa mimba na Mario Lacchin aliyekuwa katika miaka ya 50 wakati huo

Punde baada ya Losirkale kujifungua mnamo 1989, kasisi huyo alihamishwa eneo nyingine huku mamake Erobon akiozwa kwa dereva wa Lacchin, Benjamin Ekwam, aliyesajilishwa kama baba mtoto kwenye cheti za uzazi.

Kulingana na cheti changu, ni kana kwamba naishi maisha yasiyofaa, uongo. Ninataka tu kuwa na utambulisho wangum historia,” alisema Erobon jinsi alivyonukuliwa na Washington Post.

Hata hivyo safari ya kupata ukweli imekuwa ndefu na ya uchungu kwa Erobon ambaye juhudi zake za kumfikia Lacchin, 83, zimeambulia patupu.

Erobon alijaribu kuwasiliana na kasisi huyo kupitia baruameme kadha mnamo 2013 mamake alipofariki, lakini hakupata jibu lolote.

Kukutana

Kijana huyo hakufa moyo maadamu alikusudia kukutana ana kwa ana na Lacchini Marsabit alipokuwa akifanya kazi kama msimamizi wa kanisa.

Kasisi huyo alikataa kukutana naye huku akimtaka Erobon kuwasilisha malalamishi yake kwa askofu ambapo Erobon hakuwa na hiari ila kumgeukia Vincent Doyle, mtoto wa kasisi na wakili anayetetea watoto wa makasisi.

Kulingana na Erobon ambaye amejua tu aibu, kutengwa na kudhihakiwa tangu kuzaliwa kwake kutokana na maumbile yake tofauti, anachotaka tu ni ukweli kuhusu asili yake na usaidizi kutoka kwa anayedai kuwa babake kumwezesha pamoja na watoto wake wawili kutambuliwa kama raia wa Italy.

“Walibuni kitu ambacho si asili yangu halisi. Nataka tu kuwa na asili yangu, historia, ili watoto wangu vilevile wawe na asili yao halisi, utamaduni wao, historia a kila kitu” alisema.