Michezo

Mkenya anaswa na dawa za kulevya Ghana

February 28th, 2018 1 min read

Ivy Mugure Daniel, 26, aliyenaswa na dawa za kulevya nchini Ghana. Picha/ Geoffrey Anene

Na GEOFFREY ANENE

MWANAMKE mmoja kutoka Kenya ametiwa nguvuni nchini Ghana kwa ulanguzi wa dawa za kulevya za Kokain na Heroin zenye thamani ya Sh9, 143,910.

Tovuti ya My Joy Online imeripoti Jumanne kwamba Shirika la Kukabiliana na Mihadarati nchini Ghana (NACOB) lilimnasa Ivy Mugure Daniel, 26, na dawa hizo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kotoka jijini Accra mnamo Januari 9, 2018 baada ya tu ya kuwasili kutoka kwa ndege ya kampuni ya Ethiopian Airline.

“Mfuko wake ulichunguzwa na kupatikana na mzigo mwingine ndani uliokuwa umefunikwa na mfuko wa plastiki mweusi ukiwa na bidhaa ya ungaunga yenye uzito wa kilo tatu.

“Baada ya unga huo kufanyiwa ukaguzi na Halmashauri ya Ubora ya Ghana, iligunduliwa kwamba bidhaa hiyo ni mchanganyiko wa dawa za kulevya za Kokain na heroin zilizo na bei ya dola 90,000 za Marekani,” taarifa hiyo ilisema.

Baada ya kuhojiwa, mshukiwa huyo alikiri kosa lake na kukubali mzigo huo ulikuwa wake, lakini bila ya maelezo zaidi.

Alisema kwamba mpenzi wake kwa jina Benson, nchini Kenya, alimnunulia tiketi ya ndege na kumpa mfuko huo apakie vitu vyake na kumueleza wakutane Ghana akiwa na mfuko huo.

Kulingana na tovuti hiyo, Mugure amefikishwa mahakamani na kuzuiliwa akisubiri kushtakiwa.