Makala

Mkenya asakwa awanie taji la mwenye kucha ndefu zaidi duniani

May 7th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

NDOTO ya mwanamume kuvunja rekodi ya dunia kwa urefu wa kucha zake yakaribia kutimia baada ya shirika la Guinness World Records Ltd kuanza kumsaka.

Shirika la Guinness World Records, ambalo hufuatilia, kunakili na kuhifadhi orodha ya watu wanaovunja rekodi za dunia kwa matukio mbalimbali, lilisema linamsaka Mkenya huyo, John Waweru, ambaye alihojiwa na Taifa Leo mwaka wa 2013.

Wakati huo, Bw Waweru, akiwa na umri wa miaka 33, alikuwa na kucha zenye urefu wa futi 1.4 ambazo aliamini ndizo ndefu zaidi nchini na barani Afrika kwa jumla.

Bw Waweru alisema azma yake ilikuwa ni kuchukua taji la maonyesho ya kucha ndefu zaidi duniani na kuingia kwenye sajili ya Guinness World Records.

Taifa Leo ilikutana na Bw Waweru zaidi ya miaka 10 iliyopita kwenye maonyesho ya kilimo cha kimataifa huko Mkomani, Mombasa.

“Nimekuja hapa kuonyesha Wakenya kucha zangu ambazo nilianza kuzifuga miaka kadhaa iliyopita azma yangu ikiwa kuvunja rekodi ya Mwafrika mwenye kucha ndefu zaidi duniani na kuingia Guinness World Records,” alisema alipohijiwa na Taifa Leo mnamo 2013.

Shirika la Guinness World Records Ltd sasa linamtaka Bw Waweru kujitokeza kuwania taji hilo.

“Tunamtaka ajiandikishe kwenye shindano hili, huenda akavunja rekodi,” afisa wa utafiti wa talanta kwenye shirika la Guinness World Records Ltd, Charlie Anderson, aliiambia Taifa Leo kupitia barua pepe.

Anderson aliwataka Wakenya wengine wenye kucha ndefu kama za Bw Waweru kujitokeza pia kuwania taji hilo. Hata hivyo, alisema hatua ya kumsaka Bw Waweru haimaanishi kuwa tayari amevunja rekodi hiyo na hivyo kuingia kwenye Guinness World Records.

“Kwa sasa tunamsaka tu ili ajiorodheshe, lakini siwezi kutoa habari zaidi kuhusu suala hili au kuhusu endapo mtu akiibuka mshindi anapewa tuzo gani,” aliongeza kwa kusisitiza kuwa Mkenya huyo huenda akaibuka mshindi endapo atatimiza matakwa ya shirika hilo.

“Ni matumaini tu. Lakini Bw Waweru na mtu mwingine yeyote mwenye kucha ndefu anaweza kujitokeza kushiriki shindano hili na kuwania taji,” alisema Anderson.

Bw Waweru alikuwa akipokea kati ya Sh2,000 hadi Sh10,000 kwa siku kwenye maonyesho ya kucha zake jijini Mombasa.

Alikuwa amepaka kucha hizo rangi za bendera ya Kenya kusherehekea miaka 50 ya nchi yake kujitwalia uhuru kutoka kwa Wakoloni. Alisema wazazi wake walimuonya kuhusu ufugaji wa kucha zake huku majirani wakidai kuwa ana mashetani.

“Lakini wazazi wangu walibadilisha nia nilipoanza kupata riziki kutokana na kucha zangu. Nilianza kuzifuga kwa sababu nilikosa ajira baada ya kukamilisha masomo yangu ya kidato cha nne. Nikaamua kufuga kucha,” alisema.

Lakini ili kuhakikisha kwamba kucha hizo zinamea haraka, ilibidi aache kubugia pombe na badala yake kunywa maziwa na maji mengi.