Habari Mseto

Mkenya atekwa nyara Dar es Salaam

June 28th, 2019 1 min read

Na AMINA WAKO

MFANYABIASHARA Mkenya, Bw Raphael Ongangi alitekwa nyara Jumatatu usiku mjini Dar es Salaam, Tanzania akiwa na mke wake.

Kisa hicho kilitokea saa tatu unusu usiku wakati Bw Ongangi na mkewe, Bi Veronica Kundya walipokuwa wakienda nyumbani.

Ilisemekana watu watatu wenye bunduki waliwavamia kwenye makutano ya barabara za Karume na Msasani, mtaa wa Oysterbay, karibu na ubalozi wa Uganda nchini humo.

Wavamizi hao waliingia kwenye gari la wawili hao na kumlazimisha Veronica kukalia kiti cha nyuma, kisha wakachukua usukani na kuwapeleka hadi katika Ufuo wa Safari karibu na soko la samaki la Msasani.

Video zilizonaswa kwenye kamera za CCTV katika eneo la mkasa zilionyesha kulikuwa na magari matatu, pikipiki mbili na wanaume zaidi wakiwasili wakati mmoja na gari la wawili hao aina ya Land Rover Discovery Sport.

Walimwingiza Bw Ongangi kwenye gari lingine na wakaondoka na mke wake katika gari tofauti.

Duru zilisema Veronica aliachiliwa na akaamrishwa kusubiri maagizo zaidi kutoka kwa watu hao wasiojulikana.

Baadaye walimpigia simu na kumwambia asipige ripoti kwa polisi wala kwa mtu mwingine yeyote bali aende nyumbani mara moja.

Hata hivyo Veronica alipiga ripoti kuhusu utekaji nyara katika kituo cha polisi cha Oysterbay na baadaye kwa ubalozi wa Kenya nchini Tanzania.

Kufikia Alhamisi, wavamizi hao walikuwa hawajawasiliana na familia ya Bw Ongangi.

Mkenya huyo amekuwa akifanya biashara ya uchukuzi kati ya Dar es Salaam, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Zambia na Rwanda.

Ingawa kiini cha utekaji nyara huo hakijabainika, ni kisa ambacho kimetokea wakati kuna mjadala mkali kuhusu uhusiano wa Kenya na Tanzania kibiashara hasa kwa wafanyabiashara wadogo.

Mjadala huo uliibuka kufuatia malalamishi makali ya Mbunge wa Starehe, Bw Charles Njagua kwamba Kenya imekuwa karimu kupita kiasi kwa raia wa kigeni.