Michezo

Mkenya aweka rekodi mpya Amerika Kusini mbio za kilomita 42

September 24th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Emmanuel Saina alitangaza kuwasili kwake katika mbio za kilomita 42 kwa kishindo baada ya kutwaa taji la Buenos Aires Marathon nchini Argentina kwa rekodi mpya ya Amerika ya Kusini ya saa 2:05:21 mnamo Septemba 23, 2018.

Saina, 26, ambaye hakuwa ameshiriki mashindano yoyote ya marathon, aliongoza kutoka mwanzo hadi utepeni katika mbio hizi zilizovutia zaidi ya washiriki 9, 000.

Alifuta rekodi ya saa 2:09:46 ambayo Mkenya Barnbas Kiptum aliweka mwaka 2017. Kiptum pia alishiriki makala haya ya 34. Alikuwa bega kwa bega na Saina hadi kilomita 30 pale alipoachwa kabisa na kuridhika na nafasi ya pili kwa saa 2:09:19.

Raia wa Peru Christian Pacheco alifuata katika nafasi ya tatu (2:11:19) na Derlis Ayala akanyakua nafasi ya nne kwa rekodi mpya ya kitaifa ya Paraguay ya saa 2:13:41. Mkenya Godfrey Kosgei alifunga tano-bora (2:14:00). Marius Kipserem kutoka Kenya, ambaye alikuwa amepigiwa upatu kuibuka mshindi, alijiuzulu katika nusu ya pili ya mbio.

Taji la wanawake pia lilinyakuliwa na Mkenya Vivian Kiplagat Jerono. Aliibuka mshindi kwa rekodi mpya ya Buenos Aires Marathon ya saa 2:29:03. Jerono alifuta rekodi iliyokuwepo ya saa 2:30:33, ambayo Muethiopia Abeba Gebrene alitimka mwaka 2015.

Mkenya Leah Jerotich alikamilisha katika nafasi ya pili (2:32:58) naye Muethiopia Amelework Bosho akaridhika katika nafasi ya tatu (2:34:56).