Habari Mseto

Mkenya kuishi jela baada ya kutapeli Waamerika akiwaahidi kuwapa mikopo


MWANAMUME Mkenya ambaye aliondoka nchini na kwenda kufanya kazi Amerika miaka 36 iliyopita ataishi jela maisha yake yaliyobaki baada ya kupatikana na hatia ya mashtaka yanayohusiana na ulaghai.

Paul Maucha, 59, alihukumiwa na mahakama ya Amerika kutumikia kifungo cha miezi 135 gerezani na kutozwa faini ya zaidi ya dola milioni 2.1 (Sh271.1 milioni).

Mwanamume huyo ambaye sasa atatumikia takriban miaka 11 na miezi mitatu jela alihukumiwa Juni 11 na Jaji wa Mahakama ya Amerika Carl J. Nichols.

Alikuwa ameshtakiwa kwa ‘kuhusika na makosa yanayohusiana na njama ya uwekezaji’. Hii ni aina ya ulaghai wa kifedha ambapo waathiriwa wanadanganywa kulipa kiasi fulani cha pesa kwa kampuni kwa kisingizio kwamba baadaye wangepokea mikopo ya mamilioni au manufaa mengine.

Taarifa kutoka stakabadhi za mahakama zilizoonekana na Taifa Dijitali zinaonyesha kuwa Aprili 27, 2021, alifunguliwa mashitaka na mahakama akiwa na shtaka moja la kula njama ya kufanya udanganyifu, makosa matatu ya ulaghai na mawili ya kushiriki katika uhamishaji wa  mali inayotokana na uhalifu.

Alishtakiwa pamoja na mshukiwa mwenza wake Melisa Shapiro. Mahakama iliamini kwamba wawili hao walifanya walitoa habari za uwongo kwa waathiriwa waliolengwa kuhusu kampuni waliyokuwa wakiidhibiti  American Eagle Service Group Inc (AESG) ili kushawishi kwa njia ya ulaghai malipo kutoka kwa wakopaji, wakopeshaji na wawekezaji.

Wachunguzi walifahamisha mahakama kwamba waathiriwa walifikiwa na ahadi za ufadhili na fursa za uwekezaji kupitia AESG na mashirika yake yanayohusiana kwa sharti walipe ada mapema.

“AESG iliwahadaa waathiriwa kwamba ada za mapema zingeweza kurejeshwa ikiwa AESG  hangewapa  mkopo. Kama ilivyothibitishwa katika kesi, Maucha na mshiriki mwenzake walijua kuwa AESG haikuwa na mtaji wa kutoa mikopo hii na waathiriwa hawangehakikishwa  kurudishiwa pesa zao kwa sababu Maucha  mwenzake walikuwa wakigawanya ada kati yao wenyewe na kuzitumia.

“Hakukuwa na pesa za kurejeshwa,” wapelelezi hao walisema.

Stakabadhi za kesi zinaonyesha kwamba Maucha alikamatwa Mei 12, 2021 na uraia wake pia ukawa suala la wasiwasi baadaye.

Alikuwa ameachiliwa akisubiri kesi kusikilizwa kwa masharti ambayo ni pamoja na kwamba hangekiuka sheria za jimbo na kusalimisha pasipoti yake, hatapokea pasipoti au hati nyingine yoyote ya kusafiri ya kimataifa na angekaa ndani ya Columbia eneo la Maryland na Virginia. Takriban miaka miwili baadaye, serikali iliiomba mahakama kumzuilia, kwa madai kuwa alikiuka sharti lililomtaka kutotenda uhalifu.

Serikali ilisema kwamba Maucha alifanya uhalifu alipotoa taarifa za uongo kwa afisa wa Huduma ya Upelelezi ambaye alimhoji kwa kudai kwamba alizaliwa New York na ni raia wa Amerika.

Hata hivyo, ombi la serikali lilitupiliwa mbali na Mahakama mnamo Juni. 2, 2023. Badala yake, iliamriwa aachiliwe chini ya masharti yaliyorekebishwa ya kifungo cha nyumbani.

Serikali, bila kuridhika na agizo hilo, ilifaulu kukata rufaa ambayo ilisababisha kuzuiliwa kwa Maucha akisubiri kesi ilipothibitishwa kwamba Maucha alihamia Amerika kwa visa ya Mfanyakazi wa Muda Julai 1988 ambayo ilikuwa halali hadi Aprili 1989. Alitambuliwa kama raia wa Kenya aitwaye Paul Modi Maucha katika rekodi ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Amerika, na hakuwahi kuondoka nchi hiyo tangu wakati huo.

“Baada ya kuchunguza rekodi za Idara ya Usalama wa Taifa na Wizara ya Mambo ya Nje, serikali haikuthibitisha kuwa Maucha alirekebisha hali yake ya uhamiaji au  kuondoka Amerika baada ya kuingia,” mahakama iliarifiwa.

Ilizidi kufichuliwa kuwa uraia wake ulithibitishwa kutokana na machapisho katika akaunti yake ya Facebook kuhusu utambulisho wa mamake na vilevile cheti cha ndoa ambacho kilionyesha kuwa wazazi wake walizaliwa nchini Tanzania.

Akizungumzia hukumu hiyo, Keri Farley, Afisa wa FBI Atlanta, alisema inapaswa kuwa onyo kwamba shirika hilo litaendelea kuchunguza uhalifu na kuhakikisha kuwa wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

“Ulaghai wa uwekezaji unaweza kuwa mgumu kuchunguza na kushtaki kutokana na hali ya kimataifa ya shughuli za uhalifu. Lakini hukumu hii inafaa kuwa onyo kwamba FBI itaendelea kuchunguza uhalifu wa aina hii na kuhakikisha kuwa wahusika wanashtakiwa kwa mujibu wa sheria,” akasema Farley.