Habari Mseto

Mkenya nchini Bahrain asema anafanya kazi kama kawaida

April 8th, 2020 2 min read

 

Na GEOFFREY ANENE

Bahrain inafahamika kuwa mojawapo ya mataifa ambayo wanariadha wengi kutoka Kenya wamekuwa wakikimbilia barani Asia kutafuta maisha mazuri.

Hata hivyo, kuna Wakenya tu wengi ambao wanafanya kazi tofauti kabisa na riadha nchini humo. Mwandishi huyu alitafuta maoni kutoka kwa Mkenya mmoja, ambaye anafanya kazi ya karani wa mapokezi. Ni mojawapo ya kazi mtu anafaa kujikinga vizuri sana dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona kwa sababu anakutana na watu wengi.

Bahrain imeshuhudia visa 756 vya maambukizi ya corona na vifo vinne kutokana na virusi hivyo hatari vinavyohangaisha dunia nzima.

Emmanuel Amakobe Angatia amekuwa nchini Bahrain kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi 10. Alisimulia Taifa Leo kuhusu anavyojiweka salama dhidi ya maambukizi na pia kusihi Wakenya waheshimu amri ambazo serikali imetoa ili kuzuia uenezaji wa virusi vya corona.

“Mimi ni Mkenya. Ninaishi katika kisiwa cha Amwaj, eneo la Muharraq jijini Manama katika nchi ya Bahrain. Hapa tunatumia lugha ya Kiingereza kwa mawasiliano yetu. Naishi pekee yangu. Familia yangu iko nchini Kenya. Nafanya kazi na kampuni ya Kooheji Contractors kama karani wa mapokezi. Tuko Wakenya 10 katika kampuni hii.  

Tangu mkurupuko wa virusi vya corona, kampuni yangu imehakikisha tuna vifaa vya kunawa mikono (sanitizer) katika sehemu mbalimbali ikiwemo katika eneo la kupokea watu ninakofanya kazi. Kila mara nahitajika kuwa nimevalia barakoa na glavu na kudumisha usafi wa hali ya juu.

Mimi binafsi sijaathirika na janga la virusi vya corona kwa sababu kazi yangu inaendelea kama kawaida. Kwa jumla, kisiwa cha Amwaj kina wakazi ambao ni wataalamu katika nyanja mbalimbali kutoka Bara Ulaya, Asia na nchi ya Marekani.

Kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona, serikali ya Bahrain ilipiga marufuku watu kutumia sehemu za umma kama maeneo ya kufanya mazoezi ya viungo (jimu) na bustani za kustarehe, mikusanyiko ya watu na shughuli zingine zote kwa muda usiojulikana.

Wakati siko kazini, mimi nasalia kwenye nyumba nikilala na kutazama mtandao wa YouTube. Napenda Injili sana. Uzuri wa Bahrain ni kuwa kuna uhuru wa kuabudu. Makanisa ni mengi sana hapa, hasa makanisa ya kisasa.

Ningependa kushauri Wakenya wenzangu nchini Kenya kuwa wafuate maagizo waliyopewa na serikali na Shirika la Afya Duniani (WHO) na waonyeshe tabia nzuri. Nimejaa matumaini kuwa wakifanya hivi, hali hii ngumu itapita bila madhara makubwa.”