Michezo

Mkenya Wanjiru Karani ateuliwa kuhudumu katika chama cha tenisi Afrika

May 12th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Wanjiru Mbugua Karani ameteuliwa kuhudumu katika Tume ya Wanawake ya Chama cha Tenisi barani Afrika (CAT), ambayo makao yake ni nchini Tunisia.

Wanjiru, 45, ni Mkenya wa kwanza kuhudumu katika tume hiyo ya watu saba.

Tume hiyo inaongozwa na Mtunisia Salma Mouelhi-Guizani (Rais) nao Wanjiru (Kenya), Sallah Adjoa (Togo), Rashika Aboushousha (Misri), Aida Baira (Algeria), Philippina Frimpong (Ghana) na Fatime Kante (Ushelisheli) ni wanachama.

“Kila mmoja wetu alituma ombi na kuteuliwa kuhudumu kwa kipindi cha mwaka 2020 na 2021,” Wanjiru alieleza Taifa Leo hapo Jumatatu akisema ni heshima kubwa kupata kuhudumia wanatenisi wanawake kupitia kwa cheo hicho kipya.

“Ni wadhifa muhimu sana kwa sababu majukumu yetu kama watu wa kwanza kuhudumu katika tume hii yatakuwa kuimarisha mchango na majukumu ya wanawake katika mchezo wa tenisi,” aliongeza.

Tenisi ya Kenya, anasema, imekuwa katika mstari wa mbele katika kupatia makocha na wasimamizi wanawake nguvu na utoaji wa nafasi sawa.

“Kuhudumu katika kamati hiyo kutaniwezesha kupata ujuzi zaidi wa kuwapa nguvu wachezaji wa tenisi wanawake nchini Kenya na kuwafungulia milango zaidi ya kushiriki michezo,” alisema Wanjiru, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Tenisi Kenya (Tennis Kenya) kwa kipindi cha miaka mitano sasa.

Wanjiru aliwakilisha Kenya kimataifa katika michezo ya chipukizi na pia watu wazima kabla ya kustaafu na kuingilia ukocha na usimamizi wa tenisi.

Yeye pia ndiye Mkenya wa kwanza kuhudumu katika Kamati ya Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) inayoshughulikia masuala ya usawa wa jinsia. Aliteuliwa kuhudumu katika ITF mnamo Desemba 2019.