Michezo

Mkewe Alvaro Morata atisha kumtema akipoteza penalti tena

February 12th, 2018 2 min read

Straika wa Chelsea Alvaro Morata mwenye mazoea ya kufuma penalti hewa. Picha/ Hisani

Na CHRIS ADUNGO

Kwa Muhtasari:

  • Alice alilitoa tishio hilo ambalo kwa sasa ni la pili, baada ya Watford kuwatafuna Chelsea 4-1
  • Mwanamke huyo anatazamia kuhesabu rasmi ‘mabao’ mawili yaliyofungwa na Morata mnamo Machi 2018
  • Morata alimfanya Alice kuwa wake wa halali mnamo Juni 2017 kwenye sherehe za harusi
  • Staa huyo alikiri kwamba angali anammezea mate Maria aliyeanza kumwonjesha asali mnamo 2012

KATIKA jitihada za kuchangia ufufuo wa makali ya Alvaro Morata uwanjani, kidosho Alice Campello ambaye ni mkewe fowadi huyo wa Chelsea na timu ya taifa ya Uhispania, ametishia tena kuomba talaka iwapo Morata atapoteza mkwaju wowote wa penalti kabla ya kipenga cha mwisho cha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kupulizwa.

Alice alilitoa tishio hilo ambalo kwa sasa ni la pili, mwanzoni mwa wiki iliyopita baada ya Watford kuwatafuna Chelsea kama Big-G uwanjani Vicarage Road.

Kichuna huyo aliwahi kughadhabishwa sana na hatua ya Arsenal kutia kapuni ubingwa wa Community Shield mwanzoni mwa msimu huu baada ya Morata aliyesajiliwa kutoka Real Madrid kuipoteza penalti yake.

 

Penalti za chumbani

“Nayafahamu makali na uzito wa makombora ya Morata kila anaposhiriki nami michezo ya chumbani. Nataka sana kwa sasa awaonjeshe makipa wa vikosi pinzani upekee wa mikwaju yake hiyo, ila mara hii akiwa uwanjani,” alitishia Alice ambaye kwa sasa ni mjamzito.

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na magazeti mengi ya Uhispania, Alice, 22 anatazamia kuhesabu rasmi ‘mabao’ mawili aliyofungwa na Morata mnamo Machi 2018.

Hata hivyo, alisema kilele cha ujio wa watoto hao ni kumpata Morata akijivunia fomu ya kutisha kambini mwa Stamford Bridge ili kujipa uhakika wa kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Uhispania kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi hapo Juni.

Anapojiandaa kupokea vimalaiki viwili, Alice ambaye ni mwanamitindo mzawa wa Italia, alijitosa katika mtandao wake wa Instagram na kubainisha furaha ya kuitwa mama baada ya kuandamana na mumewe jijini London kununua baadhi ya bidhaa za malezi ya mtoto wiki iliyopita.

 

Busu hadharani

Kwenye video iliyoipakia, videge hao walionekana wakibusiana peupe walipokuwa wakitokea katika duka la Pure Baby, London kabla ya kushikana mikono na kuzivisha nyuso zao tabasamu tele.

Morata, 25, alimfanya Alice kuwa wake wa halali mnamo Juni 2017 kwenye sherehe za harusi zilizoandaliwa katika ukumbi wa Basilica del Redentore jijini Venice, Italia.

Kabla ya kufunga silisili za maisha na Alice ambaye pia ni gwiji wa fasheni za mavazi ya kike, Morata alikuwa amekiri kwamba bado ‘anateswa hisia’ na tukio la kutemana na Maria Pombo, kipusa aliyechumbiana naye kwa miaka miwili kabla ya kumpata Alice mwanzoni mwa 2015.

Katika mahojiano tofauti kati yake na gazeti la udaku la Chi jijini Turin, Italia, Morata alikiri kwamba angali anammezea mate Maria aliyeanza kumwonjesha utamu wa asali mnamo 2012.