Dondoo

Mkewe bosi atimua kidosho akidai atampokonya mume

December 12th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Viwandani, Nairobi 

Mke wa mkurugenzi wa kampuni moja eneo hili aliwashangaza wafanyakazi alipomlazimisha kipusa kurudi nyumbani kubadilisha nguo akidai alinuia kumteka mumewe kimapenzi. ?

Inasemekana mwanadada aliamua kumfukuza mrembo huyo akihofia kuwa huenda angempokonya mume wake.

Penyenye zinasema mwanadada alikuwa amesikia habari kumhusu mrembo huyo na mavazi yake na aliamua kupitia kazini ambapo walikutana ana kwa ana. “Mbona unapenda kuvalia hivi?” alimuuliza mrembo.

Kwa kuhofia kufutwa kazi, mrembo aliamua kunyamaza.

Penyenye zinasema mke wa mdosi alikuwa akichunguza mienendo ya mrembo yule kisiri kwa muda baada ya kupata habari kuhusu mitindo yake ya mavazi.

“Mbona ni wewe peke yako unayevalia hivi kila siku? Ama mdosi wako alikupa idhini ya kuvaa hivyo?” mwanadada alitaka kujua.

Duru zinasema ilibidi kidosho kumjibu. “Hizi nguo ndizo chaguo langu. Sivai hivi kumpendeza wala kumvutia yeyote,” mrembo alimueleza mke wa mdosi wake.

Kulingana na mdokezi, maneno ya mrembo hayakumridhisha mke wa bosi. “Wewe utaacha ukora. Nia yako naijua. Unavalia hivi ukitaka kumteka bwanangu,” alimshtumu mrembo.

Wafanyakazi wa kampuni hiyo walibaki kushangaa lakini hawakusema lolote.

“Wewe ni wale wenye nia ya kuvunja ndoa za watu. Yangu hautoboi,” mwanadada aliapa.

Inadaiwa alimpa mrembo dakika tano kurudi kwake abadilishe nguo la sivyo atimuliwe kazini.

“Sitakuruhusu uendelee kukaa hapa na hizi nguo zako. Hata hizo nywele toa. Fanya hivyo haraka,” mwanadada alimueleza mrembo.

Mrembo alibaki mdomo wazi. “Nimesema toka hapa haraka. Shika njia na usirudi hapa tena ikiwa hautabadilisha mavazi yako,” alisema na kuwaita walinzi kumtimua kidosho.