Habari MsetoSiasa

Mkewe Trump kuzuru Kenya Oktoba

September 26th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MKEWE Rais wa Amerika Donald Trump, Melania Trump amepangiwa kuzuru Kenya mwezi Oktoba atakapozuru mataifa kadha ya Afrika.

Akihutubu Jumatano, Bi Trump alisema atakuwa akizuru mataifa manne “mazuri na yenye sifa za kipekee” barani Afrika ambayo ni; Ghana, Malawi, Kenya na Misri.

Ziara hiyo ni yake ya kwanza barani Afrika tangu mumewe alipochukua hatamu za uongozi wa Amerika mnamo Januari 20 mwaka jana.

“Hii ndio itakuwa ziara yangu ya kwanza barani Afrika na ninafurahi kwamba nitajifunza mengi kuhusu masuala yanayowaathiri watoto katika bara hilo. Pia nitajifahamisha na utajiri wake mkubwa katika nyanja ya utamaduni na historia,” Bi Melania alisema katika mahojiano yake ya awali.

“Sisi ni wanajamii wa dunia na ninaamini kuwa kwa njia ya mazungumzo na kubadilishana mawazo tutapata nafasi ya kufunzana mengi,” akaongeza.

Mama huyo wa Taifa wa Amerika atafanya ziara hiyo peke yake bila kuandamana na mumewe.

Melania alitaja mataifa ambayo atazuru wakati wa halfa iliyoandaliwa kwa heshima ya wake za viongozi wakuu ulimwenguni wanaohudhuria Kongamano la 73 ya Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Amerika.

Ziara hiyo itafanyika miezi miwili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru Amerika kwa mwaliko maalum wa Rais Trump. Rais Kenyatta na mwenyeji wake walijadiliana masuala kadhaa yenye umuhimu kati ya Kenya na Amerika, kama vile biashara, uwekezaji, utalii na usalama.

Tarehe kamili ya ziara ya Bi Trump nchini haijabainishwa japo duru zinasema itafanyika “mapema mwezi Oktoba”.