MKF yawataka wanasiasa kuheshimu Rais Kenyatta wanaposaka kura

MKF yawataka wanasiasa kuheshimu Rais Kenyatta wanaposaka kura

Na SAMMY WAWERU

WAKFU wa wafanyabiashara kutoka Mlima Kenya unaofahamika kama Mount Kenya Foundation (MKF) umewataka wanasiasa wanaotofautiana na Rais Uhuru Kenyatta kukoma kumrushia cheche za matusi.

Naibu mwenyekiti wa wakfu huo, Bw Titus Ibui alisema Alhamisi Rais Kenyatta ni zaidi ya msemaji wa jamii ya eneo hilo, akimtaja kuwa ‘Muthamaki’ (jina lenye maana ya aliyetakaswa, kwa mujibu wa lugha ya Agikuyu).

Bw Ibui alitoa kauli hiyo katika mkutano wa wakfu huo na vinara wa One Kenya Alliance (OKA), ulioandaliwa jijini Nairobi.

OKA inajumuisha, Mabw Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (KANU).

“Vinara wa OKA tumekutana na tumezungumza, ila kuna jambo moja tu tunawaomba kama wanasiasa; mheshimu rais wetu,” Bw Ibui akasema.

Mfanyabiashara huyo aidha alitoa onyo kwa wanasiasa, akisema MKF haitaruhusu kiongozi wa nchi kurushiwa cheche za matusi.

“Wanasiasa msipoheshimu rais, kumrushia cheche za matusi na kumuita majina, watu wa Mlima Kenya hawatakubali kwa sababu angali msemaji wao,” akatahadharisha.

Wiki iliyopita, wakfu huo ulikutana na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na Ibui alidokeza Alhamisi kwamba haujatoa maamuzi ya ni nani utakayeunga mkono kuwania kiti cha urais mwaka 2022.

“Hatujatangaza chaguo letu. Juma lililopita pia tulifanya mkutano na Bw Raila Odinga. OKA tumewapa ufunguo wa Mlimani, mjitume kuuza sera zenu,” akasema.

Alisema muungano huo utatoa tangazo baadaye, baada ya kutathmini sera na ajenda za wanaomezea mate wadhifa wa urais 2022.

Eneo la Mlima Kenya limeonekana kuwa na mvuto kwa viongozi na wanasiasa waliotangaza nia yao kuwania urais.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa mkate wa maziwa

Wanamichezo bora Kenya mwaka 2021 kutuzwa katika kaunti ya...