Michezo

Mkimbiaji Mkenya apigwa marufuku kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli

September 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI wa masafa marefu wa Kenya, Patrick Siele amepigwa marufuku miaka mitatu na miezi sita Alhamisi baada ya kuhepa maafisa wa kupima matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Kitengo cha Maadili cha Shirikisho la Riadha Duniani (AIU) kinasema kuwa Siele, ambaye alizaliwa Julai 27 mwaka 1996, amepokea adhabu hiyo baada ya kukwepa, kukataa kupimwa ama kukataa kupeana sampuli ya damu ama mkojo kupimwa, ambayo ni ukiukaji wa sheria za kukabiliana na matumizi ya pufya.

Marufuku ya Siele inaanza kuhesabika kutoka Machi 16 mwaka 2020. Mbali na kupigwa marufuku, Siele pia amepoteza matokeo ya mbio zote ameshiriki kutoka Desemba 18, 2019 hadi mwaka 2020. Anakubaliwa kukata rufaa dhidi ya adhabu hiyo.

Siele ni Mkenya wa tisa kupatikana upande mbaya wa sheria mwaka 2020 baada ya Peter Kwemoi, Vincent Yator, Mike Kiprotich Mutai, Japhet Korir na Wilson Kipsang’ (miaka minne kila mmoja), Kenneth Kipkemoi (miaka miwili) na Philip Cheruiyot Kangogo (miaka miwili), Alex Korio Oloitiptip (miaka miwili) na Mercy Kibarus (miaka minane).