Habari Mseto

Mkinzano katika kesi ya NHIF

December 10th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alieleza mahakama ya kuamua kesi za ufisadi kuwa wakuu 21 katika hazina ya kitaifa ya bima (NHIF) walifanya makosa mabaya sawa na ya kuua kwa kuiba pesa za kufadhili matibabu ya wagonjwa kote nchini.

“Naomba hii mahakama iwaachilie washtakiwa hawa kwa masharti makali ya dhamana kwa vile wamefanya makosa mabaya kuliko ya kuua,” alisema naibu wa DPP Bi Emily Kamau.

Bi Kamau alimweleza hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti kuwa dhamana ni haki ya washtakiwa lakini akasema “ washukiwa hawa walisababisha wagonjwa wengi kukata roho mahospitalini kwa kukosa pesa za matibabu.”

Matamshi hayo ya Bi Kamau yalisababisha malumbano makali kati yake na mawakili wanaowatetea washtakiwa.

Bw Cliff Ombeta alimfokea Bi Kamau na kumweleza , “ Hakuna ushahidi wowote wa wagonjwa waliokufa kwa kutopata ufadhili.

Bw Ombeta alimweleza kiongozi huyo wa mashtaka (Kamau) asipotoshe mahakama kwa lengo la kutaka ombi lao la dhamana liwekwe masharti makali.

Bi Kamau alimsihi hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti atilie maanani pesa zilizofujwa na washtakiwa hao 21 na kusisitiza,” wakenya waliofariki kutokana na wizi uliotekelezwa na washtakiwa ulisababisha wengi kufariki kwenye mahospitali kwa kukosa fedha za kugharamia matibabu yao.”

Walioshtakiwa ni aliyekuwa kinara wa NHIF Simeon Lemminte ole Kirgotty, aliyekuwa mkurugenzi mkuu Geoffrey Gitau Mwangi, wakili wa NHIF Ruth Sudoi Makallah, Pamela Nyaboke Marendi, Joseph Mutinda Mbuvi, David Muli Nzuki, Gibson Kamau Muhuhu, Irene Ng’etich Rono, Jacinta Nyakio Mwangi,  Gilbert Gathuo Kamau, Kennedy Arthur Wakhu, Fredrick Sagwe Onyancha, Millicent Wangui Mwangi, Matilda Mwangemi, Darius Philip Mbogo, aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha kuwatetea walimu (KNUT) Mudzo Kuhenderwa Nzili , Yussuf Ibrahim, Elly Nyaim Opot,Danson Muchemi Njunji, Robert Muriithi Muna na kampuni ya Wentribe Limited.

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka mbali mbali.

Mabw Kirgotty na Mwangi, Bi Makallah na Bi Marendi walikana shtaka la kutumia vibaya pesa za NHIF kwa kuiruhusu kampuni ya Webtribe kuikusanyia pesa kutoka kwa wateja wake.

Mahakama ilifahamishwa kuwa wanne walitumia kampuni ya  Webtribe kuikusanyia NHIF Sh49,513,440.

“Naomba hii mahakama isikubali kupotoshwa na matamshi ya Bi Kamau. Hajawasilisha ushahidi wowote wa watu waliofariki kwa kukosa ufadhili wa NHIF,” alisema wakili Cliff Ombeta aliyemwakilisha Bw  Simeon Lemminte ole Kirgotty aliyekana shtaka  la ufujaji wa zaidi ya Sh550milioni.

Pia alisema baadhi ya washtakiwa ni wagongwa. Alisema Bw Kirgotty anaugua kisukari na shinikizo la damu.

Alisema Irene aliondolewa hospitali Jumatatu kushtakiwa.

“Mtoto wa Irene mwenye umri wa miezi miwili unusu ni mgonjwa. Hata Irene mwenyewe ni mgonjwa,” Bw Ogoti alifahamishwa na kuongezewa , “ kuna afidaviti inayosimulia anachougua.”

Bw Ogoti alimruhusu Irene kuondoka kumnyonyesha mtoto.

Hakimu aliwaachilia kwa dhamana ya viwango mbali mbali  kati ya Sh2milioni pesa tasilimu hadi Sh300,000 pesa tasilimu.

Washtakiwa walikanusha mashtaka 17 dhidi yao.