Mkishiriki maandamano mtahatarisha nafasi zenu kazini, COTU yaonya wafanyakazi

Mkishiriki maandamano mtahatarisha nafasi zenu kazini, COTU yaonya wafanyakazi

NA CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Wafanyakazi Nchini (COTU) umewashauri wafanyakazi kwamba wasishiriki maandamano yaliyotangazwa kuongozwa na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Jumatatu, Machi 20, 2023.

COTU inasema kuwa maandamano hayo yameratibiwa kufanyika siku ya kazi na ambayo haijatangazwa rasmi na serikali kuwa siku ya mapumziko.

“Kama muungano wa vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi, tungependa kuwakumbusha wafanyakazi kulinda nafasi zao kwa kuripoti maeneo yao ya kazi Jumatatu,” akasema Naibu Katibu Mkuu wa COTU Benson Okwaro, kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Machi 18, 2022.

“Tunaonya wafanyakazi dhidi ya kushiriki katika shughuli zozote ambazo zitahatarisha nafasi zao za ajira,” akaongeza.

COTU imetoa onyo hilo baada ya wabunge wa Azimio kuwataka waajiri wote, isipokuwa wamiliki wa vyombo vya habari, kuwaachilia wafanyakazi wao washiriki katika maandamano hayo, wakisema hilo ni “wajibu wa kitaifa”.

Wakiongozwa na kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi, wabunge hao walisema wafanyakazi waruhusiwe kutoripoti kazini “kwa sababu kiongozi wa Azimio Raila Odinga ametangaza Jumatatu kuwa siku ya mapumziko”.

“Kwa sababu Jumatatu imetangazwa kuwa siku ya mapumziko, waajiri wote isipokuwa wale katika sekta ya vyombo vya habari, wanafaa kuwaruhusia wafanyakazi wao washiriki maandamano. Tunataraji kuwa waajiri wataelewa,” Bw Wandayi, ambaye ni mbunge wa Ugunja akasema.

Lakini COTU imehimiza kufanyike mazungumzo kati ya serikali na upinzani ili kulinda uchumi wa nchi.

Hii ni kwa sababu kuna hofu kwamba huenda ghasia yakashuhudiwa wakati wa maandamano hayo baada ya baadhi ya wafuasi wa Azimio kuapa kuelekea Ikulu.

Hata hivyo, Bw Odinga na vinara wenzake wa Azimio wameshikilia kuwa maandamano yao yatakuwa ya amani na wakawataka maafisa wa polisi kuwapa ulinzi.

  • Tags

You can share this post!

Malala amtaka Ida Odinga kuandalia UDA chai na ugali siku...

Wabunge Kihara na Ichungwa wamtaka Kenyatta kutangaza...

T L