Mkitunyima huduma za serikali, basi msituombe kura – Wakenya mitandaoni

Mkitunyima huduma za serikali, basi msituombe kura – Wakenya mitandaoni

Na WANGU KANURI

WAKENYA Twitter Jumatatu wameghadhabishwa na tisho lililotolewa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe la kutowaruhusu kupata huduma za kiserikali bila chanjo kamili ya Covid-19.

Kupitia ujumbe wake, Waziri Kagwe alisema kuwa Wakenya watalazimika kuonyesha cheti cha kuchanjwa ili kupokea huduma hizo.

“Huduma hizo ni pamoja na Uhamiaji, Elimu, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA), huduma za bandari na idhini za kuwatembelea wagonjwa na wafungwa,” akaeleza.

Wakenya hawakuchelewa kuonyesha hamaki zao mitandaoni, wakitaja hatua hiyo kama isiyofaa hasa katika kipindi ambacho nchi imepata pigo kiuchumi kutokana na gonjwa hilo.

“Aidha upate KRA pini ama hutapata huduma za benki. Upate nambari ya Huduma ama hutapata huduma za serikali. Wakenya wapate chanjo ama hawatapata huduma za serikali. Lipa NHIF hata kama hujaajiriwa ama hutapata huduma za serikali. Walimu wapokee chanjo ama watachukuliwa hatua. Mutahi Kagwe, ni siku gani utasema mabilionea wa Covid warudishe pesa walizobadhiri ama waende jela?” akauliza @NahashonKimemia.

Kilichowakera zaidi ni serikali kusema itawanyimwa huduma za serikali huku wanasiasa wengi wakiendelea kupiga kampeni za uchaguzi wa 2022, wakitembea kila kona ya nchi wakiomba Wakenya kura.

“Kinaya ni kwamba Mutahi Kagwe amesema kuwa Wakenya hawatapata huduma za serikali iwapo hawatapata chanjo lakini watawaruhusu Wakenya kupiga kura mwaka ujao. Nchi hii hukutumia wakikuhitaji kisha wanakuacha,” akaandika @Bigman_ibrah.

“Ikiwa Mutahi Kagwe ameamua hivyo, basi hatupaswi kupiga kura wala kulipa ushuru. Serikali ijitegemee nasi tujitegemee,” akasema @KamauWaMwangi_.

“Mutahi Kagwe anapaswa kujua kuwa kuna watu ambao ni heri wapigwe risasi kabla hawajajiandikisha kupata chanjo ya Covid-19. Kututishia na huduma za serikali ni utoto,” akalalama @kurgatkogeyben.

“Mtu amweleze Mutahi Kagwe kuwa tunalipa ushuru ili tupate huduma. Huduma si fadhili kutoka kwa serikali,” akaandika @JaneIrunguKE.

Isitoshe, hoteli, baa na biashara zinazowahudumia zaidi ya watu 50 zitahitajika kuwaeleza wateja wao kuonyesha vyeti hivyo kuanzia Desemba 21, 2021.

Hii inajiri wakati ambapo Wakenya wanajiandaa kwa sherehe za Krismasi na mwaka upya, hali ambayo serikali inahofia huenda ikachangia kuenea kwa virusi hivyo.

Kufikia Novemba 21, 2021 ni watu milioni 6.4 wamechanjwa huku watu milioni 2.4 wakiwa wamepokea chanjo kamili. Serikali ilikuwa imenuia kuwachanja nusura watu milioni 10 ifikapo Desemba.

  • Tags

You can share this post!

Simbas kuvaana na Diables Barcelona mchuano wa mwisho...

Mourinho amnunulia mchezaji wake wa AS Roma zawadi ya viatu...

T L