Makala

Mkokoni: Mji wa mahasimu kujenga urafiki

February 28th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MKOKONI ni mmojawapo wa miji yenye sifa na historia pana Lamu.

Ni mji unaopatikana Lamu Mashariki, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Ni makazi ya watu wapatao 1,000 ambao wengi kiukweli ni Waswahili wa asili wa Wabajuni.

Kulingana na wazee na wanahistoria waliohojiwa na Taifa Leo, jina ‘Mkokoni’ linatokana na mti wa mkoko.

Msitu wa Mkoko unatambulika sana, hasa maeneo ya mwambao wa Pwani ambayo yamepakana na Bahari Hindi.

Eeneo hilo la Mkokoni lilibandikwa jina hilo kutokana na utajiri mwingi wa mikoko ipatikanayo eneo hilo hadi sasa.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, ambaye pia ni mwanahistoria, Mohamed Mbwana Shee, anasema mji huo wa Mkokoni ulipata umaarufu miaka ya sabini (1970s).

Kulingana na Bw Mbwana, mahasimu waliokuwa wakiishi mji wa kale wa Matironi walijipata wakikutana Mkokoni, hivyo kulazimika kuzika tofauti zao na kuanza maisha mapya Mkokoni.

“Mkokoni ni eneo linalosifika sana kwa kuwa na msitu wa mikoko. Mnamo 1940, Wabajuni wengi walikuwa wakiishi mji wa kale wa Matironi. Wakati huo, kulishuhudiwa migawanyiko na visirani visivyokoma, hali iliyowafanya baadhi ya Wabajuni kuhama kuepuka migogoro hiyo kuja kuishi kwa muda Mkokoni, ambapo pia palikuwa pakitumiwa kama bandari,” akasema Bw Mbwana.

Anataja kuwa mnamo mwaka 1964 wakati wa vita vya Shifta, Wabajuni waliokuwa wamebakishwa Matironi na wale waliokuwa wamehamia Mkokoni, wote walifurushwa kutoka kwa makazi yao, hivyo kukimbilia usalama wao katika kisiwa jirani cha Kiwayu.

Kuna wengine waliohamia Lamu kisiwani, Ngomeni, Watamu, Kilifi na maeneo mengine ya Pwani.

Mnamo 1970, baada ya vita vya Shifta kusitishwa, Wabajuni wote waliokuwa eneo walilohamia la Kiwayu na pia wale waliokuwa nje ya Lamu, walirudi, ambapo badala ya wengine kuelekea Matironi, wakaafikia kukongamana Mkokoni.

Ikumbukwe kuwa Wabajuni wa Matironi walikuwa awali wamekorogana na wenzao waliolazimika kuhamia Mkokoni.

Mzee Mohamed Mbwana Shee ambaye ni mwanahistoria wa Lamu. Anasema mji wa Mkokoni ulipata jina kutokana na kuwa na ukwasi wa misitu mingi ya mikoko. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mbwana anafafanua kuwa ni makundi hayo mawili ya Wabajuni yaliyokuwa na uhasama na ambayo yalikuwa yamekimbilia Kiwayu ambayo yalipiga moyo konde kuja pamoja na kuunda Mkokoni ya sasa.

“Punde vita vya Shifta kuisha, wa Mkokoni walirudi Mkokoni ilhali wale wa Matironi wakadinda kurudi kwao kwa kuhofia kuvamiwa tena na Shifta. Hapo ndipo waliafikia kuvunja uhasama wao na Wabajuni wenzao wa Mkokoni, hivyo wote wakakusanyika Mkokoni na kubuni mji mpya ambao umedumu hadi sasa. Ina maana kwamba Mkokoni ya sasa imeleta umoja wa Wabajuni wa pande mbili waliovunja mji wa kivita wa Matironi, kuzika tofauti zao na kuishi raha mustarehe na kwa pamoja Mkokoni,” akasema Bw Mbwana.

Mohamed Ali, Mkazi wa Mkokoni, anataja hatua ya Wabajuni wa Matironi na Mkokoni ya kuzika tofauti zao na kuja pamoja kuunda Mkokoni ya sasa kuwa yenye natija tele.

Bw Ali anasema Mkokoni tangu ibuniwe imekuwa kielelezo chema kwa wakazi wa miji mingine ya Lamu.

“Umoja na amani iliyoko Mkokoni huwezi kuilinganisha na miji mingine yoyote ile iliyoko Lamu au Pwani. Utasikia tofauti zikizuka ama watu kuumizana baada ya kutofautiana sehemu nyingi za Lamu lakini siyo Mkokoni. Hapa watu wamethamini vilivyo umoja na amani. Yote yanatokana na historia iliyoko kwenye mji wetu,” akasema Bw Ali.

Bi Fatma Aboud, mkazi wa Mkokoni, anataja uhusiano au umoja ulioko Mkokoni kuwa changizo kuu ya maendeleo yanayoshuhudiwa eneo hilo kila kuchao ikilinganishwa na vijiji vingine vya Lamu.

Shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa Mkokoni ni uvuvi.

Kisiwa hicho pia kimesifika sana kwa ukulima wa matikitimaji ambayo yamekuwa yakisafirishwa na kuuzwa hata kwenye kisiwa cha Lamu.

Matikitimaji kutoka mjini Mkokoni yakikaguliwa kisiwani Lamu muda mfupi baada ya kusafirishwa kwa boti. Kisiwa cha Mkokoni kinasifika kwa ukuzaji wa matikitimaji na uvuvi. PICHA | KALUME KAZUNGU