Michezo

Mkombozi Ronaldo aibeba Ureno hadi fainali ya Nations League

June 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PORTO, Ureno

CRISTIANO Ronaldo alipachika mabao matatu na kusaidia Ureno kubwaga Uswizi 3-1 na kutinga fainali ya Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya mjini Porto, Jumatano.

Ronaldo alifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 25, lakini Uswizi ikasawazisha dakika ya 57 kupitia penalti ya Ricardo Rodriguez dakika chache baada ya refa kutumia teknolojia ya VAR na kubatili uamuzi wa kuipa Ureno penalti.

Muda wa mechi ulionekana utaongezwa, lakini Ronaldo alionesha weledi wake wa kuchana nyavu kwa kukamilisha mashambulizi mawili katika dakika ya 88 kabla ya kugonga msumari wa mwisho dakika ya 90.

Wenyeji Ureno sasa watamenyana na mshindi kati ya Uingereza na Uholanzi, ambao waliratibiwa kulimana jana usiku, katika fainali siku ya Jumapili.

Ureno iliingia nusu-fainali bila ya mfungaji wake hodari Ronaldo ambaye alikuwa amechukua likizo kutoka timu ya taifa kumakinikia msimu wake wa kwanza katika klabu ya Juventus nchini Italia.

Hata hivyo, mshindi huyu mara tano wa tuzo ya mwanasoka bora duniani alirejea kusakatia Ureno mwezi Machi na alitarajiwa kuwa kivutio katika siku ambayo pia habari zilisema kwamba kesi ya ubakaji dhidi yake ilikuwa imetupiliwa mbali.

Kesi yaendelea

Wakili wa mwanamke Mwamerika aliyedai kunajisiwa na Ronaldo, ambaye amekataa madai hayo, alikanusha baadaye ripoti hizo, akisema kesi hiyo bado inaendelea.

Kwa wakati huu, nahodha huyu wa Ureno si nyota pekee katika timu ya taifa, huku Bernardo Silva akipata umaarufu Manchester City ambako huenda hivi karibuni akakaribisha Joao Felix.

City inasemekana iko tayari kulipia ada ya kuruhusu Felix aondoke Benfica ya Sh13.6 bilioni, ingawa kinda huyu mwenye umri wa miaka 19 alikosa nafasi ya wazi katika mechi yake ya kwanza kabla ya mapumziko alipopiga fyongo pasi kutoka kwa Ronaldo.

Uswizi ilibabaisha Ureno katika kipindi cha kwanza, huku Xherdan Shaqiri, ambaye majuzi alinyakua taji la Klabu Bingwa Ulaya na klabu yake ya Liverpool, akisisimua.

Hata hivyo, ilihitaji utata wa VAR kurejesha Uswizi kwenye mechi kabla ya matumaini yao kuzimwa na mabao mawili kutoka kwa Ronaldo.