Michezo

Mkongwe Emilio Nsue aongoza ufungaji mabao robo fainali Afcon ikianza Ijumaa

February 1st, 2024 1 min read

JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA

DIMBA la Afcon linaingia hatua ya robo-fainali Ijumaa na Jumamosi huku vita vya kuwania Kiatu cha Dhahabu vikichacha.

Mshambuliaji Emilio Nsue wa Equatorial Guinea ndiye anayeongoza baada ya kufunga mabao matano, yakiwemo matatu katika ushindi wao wa 4-1 wa mechi ya Kundi A dhidi ya Guinea-Bissau.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 34 anafuatwa na Gelson Dala wa Angola aliyepachika wavuni mabao manne, huku Baghdad Bouriedjah wa Algeria, Agostinho Mabululu wa Angola, Lassine Sinayoko (mali) na Bertrand Traore wa Burkina Faso wakijivunia mabao matatu kila mmoja.

Jordan Ayew, Mohammed Kudus (wote wa Ghana), Lamine Camara, Habib Diallo (wote wa Senegal), Mohamed Bayo (Guinea), Ademola Lookman na Victor Oismhen (Nigeria), Ryan Mendes (Cape Verde) na Thembe Zwane wa Afrika Kusini kila mmoja akiwa na bao moja.

Katika robo-fainali ya Ijumaa jijini Abidjan, Nigeria itaingia uwanjani ikitaka kumaliza kipindi cha miaka 10 cha ukame wa kombe hili, lakini wapinzani wao, Angola nao wanataka ushindi mbali na kuandikisha rekodi. Mechi hii itachezewa kwenye uwanja wa Houphouet Boigny jijini Abidjan kuanzia saa mbili usiku.

Robo-fainali nyingine itakutananisha DR Congo na Guinea kuanzia saa tano usiku, timu zote zikiwa miongoni mwa zilizoshangaza wengi katika michuano hii.

Timu hizi hazina rekodi kubwa, lakini kufuzu kwao kuliwashangaza wengi waliozipuuza kabla ya mashindano haya kuanza.

Ni mara ya kwanza kwa Guinea kushiriki katika mashindano haya, lakini ni mara ya 19 kwa DR Congo. Mechi hii itachezwa uwanja wa Stade de la Paix mjini Bouake kuanzia saa tano usiku.