Habari Mseto

Mkono mrefu wa sheria wamkamatia nchini Sudan Kusini

June 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MENEJA wa kituo cha Petroli aliyetoroka kwa miaka minne alishtakiwa Ijumaa baada ya kupatikana nchini Sudan kusini.

Bw Ahmed Ibrahim alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku na kukanusha  matano ya wizi wa mafuta ya petrol yenye thamani ya Sh32 milioni.

Bw Ibrahim alijitetea kuwa alizuiliwa nchini Sudan kusini  tangu 2014 alipokuwa ameenda kuekeza.

“Vita vilizuka Sudan kusini mshtakiwa akazuiliwa huko na waasi hata akawa mgonjwa. Unapomwona akisimama mbele ya korti ni mgonjwa,” wakili anayemwakilisha mshtakiwa  alimweleza hakimu.

Wakili huyo aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana akisema “ hatakosa kufika kortini.”

Bi Mutuku alielezwa mshtakiwa alitoroka tanguy 2014 kwa sababu ya  kutiwa kizuizini na waasi Sudan kusini  hadi mapema mwezi huu alipotoroka.

“ Polisi walikuwa wakimsaka mshtakiwa kila mahala na walipomwona nyumbani akiwa hafifu kwa ugonjwa walimshika na kumfikisha kortini leo Ijumaa,” alisema wakili huyo.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Aveda hakupinga ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana akisema “ polisi walikuwa wamemweleza yaliyomvika mshtakiwa.”

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh300,000 na kuamuru kesi isikizwe Julai 12, 2018.

Bw Ibrahim alikabiliwa na mashtaka kuwa kati ya Oktoba 1 na Novemba 30 2014 katika kituo cha kuuza mafuta ya Petroli cha Olympics  aliiba bidhaa mbali mbali za mafuta petrol lita 328,002 ya thamani ya Sh32,534,464.

Pia alishtakiwa kuiba mafuta ya taa  lita 24,502 yenye thamani ya Sh1,795,000 akishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa kiortini.

Shtaka la tatu lilisema kuwa akiwa katika kituo hicho cha Petroli cha Olympic kilichoko Ongata Rongai kaunti ya Kajiado akiwa meneja hakutoa riziti za mauzo ya mafuta hayo ya Sh32.5 milioni

Shtaka la nne lilikuwa alinunua lori nambari KCA 601M akitumia pesa hizo alizoiba.

Pia alishtakiwa kutumia pesa hizo za wizi kujijengea nyumba ya kuishi mtaani Bula Pesa kaunti ya Isiolo.