Makala

Mkono wa Ikulu ‘ulivyochochea’ Gavana Kawira Mwangaza kuvuliwa uongozi wa Meru      


ZIARA ya Ikulu na madai ya kuingiliwa kisiasa yamehusishwa na hatua ya Seneti kumtimua Gavana wa Meru Kawira Mwangaza, huku jaribio la dakika za mwisho  la magavana wa kike za kumuokoa mwenzao zikigonga mwamba.

Waliopanga kumtimua waliwashawishi maseneta kwa misingi ya kisiasa wakilenga kura nyingi zaidi za wale wa muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Kulingana na duru zinazofahamu njama za kisiasa zilizosababisha kutimuliwa kwa Bi Mwangaza, timu ya viongozi wa kisiasa kutoka Meru ilienda Ikulu Jumatatu ambapo waliripotiwa kumsihi Rais William Ruto kutoingilia suala hilo.

Wakiwa na ujasiri, timu hiyo ilienda kwa Seneta wa Kenya Kwanza, anayeshikilia wadhifa mkubwa wa uongozi na kumpa jukumu la kuwashawishi maseneta 28 kutoka muungano huo, idadi iliyotosha kumpeleka nyumbani Bi Mwangaza, mwenye umri wa miaka  miaka 50.

Mkakati huu ulikuwa wa kuhakikisha wamevuka hitaji la kisheria la maseneta 24 wanaohitajika kuunga mkono kuondolewa mamlakani kwa Gavana Kawira.

Bi Mwangaza alipata agizo la Mahakama kusitisha kwa muda kutimuliwa kwake.

“Viongozi walioenda Ikulu walitajwa wakati wa kusikilizwa kwa mashtaka mbele ya seneti. Walimsihi Rais asichukue msimamo kuhusu suala hilo. Hii iliwapa nguvu za kufanikisha ushawishi kwa misingi ya chama,” alisema mdokezi anayejua yaliyoendelea..

Mdokezi huyo alisema magavana wa kike walijaribu kuingilia kati kwa kuwasiliana na Rais lakini inasemekana hakuchukua msimamo wowote.

Muungano wa Kenya Kwanza una maseneta 30 baada ya maseneta sita wa United Democratic Movement na Jubilee Party kujitenga na upinzani na kushirikiana na muungano tawala, na kuongeza maseneta 24 wa United Democratic Alliance (22) na mmoja kutoka Ford Kenya na Democratic Party (DP).

Azimio kwa sasa ina maseneta 17, 13 kutoka ODM, watatu kutoka Wiper ya Kalonzo Musyoka na Seneta wa Busia Okiya Omtatah wa chama cha National Reconstruction Alliance.

Upigaji kura ulipoitishwa na Spika wa Seneti Amason Kingi, maseneta 26 walipiga kura kuunga mkono shtaka la kwanza la ukiukaji mkubwa wa Katiba na sheria zingine huku maseneta wanne wakipiga kura dhidi ya shtaka hilo na 14 wakisusia.

Maseneta hao 26 walipiga kura tena kuunga mkono shtaka la pili la utovu wa nidhamu, huku wawili pekee wakipiga kura kupinga.

Waliosusia walikuwa 14.

Katika shtaka la tatu la matumizi mabaya ya afisi, maseneta 27 walipiga kura kuunga mkono, mmoja akipinga huku 14 wakikataa kushiriki.

Hata hivyo, upigaji kura haukuendelea bila mtafaruku kwani kizaazaa kilizuka katika Seneti huku maseneta wakipiga kelele huku Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna akifikia hatua ya kumwita Spika Kingi “aibu”.

Seneta mteule Gloria Orwoba alitupwa nje ya Bunge na Spika Kingi, alipolalamikia ukosefu wa mjadala kabla ya kupiga kura.

Maseneta wa Azimio walikataa kushiriki upigaji kura na wakaungana na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, anayetoka Kenya Kwanza.