Kimataifa

Mkosoaji mkuu wa Putin afariki, katika pigo kuu kwa demokrasia Urusi

February 16th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

VIONGOZI wa mataifa ya Magharibi wa wamemlaumu moja kwa moja Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kifo cha Kiongozi wa Upinzani Alexei Navalny, huku Rais wa Amerika Joe Biden akisema, “hili ni thibitisho lingine tosha kuhusu ukatili wa Putin”.

Navalny, 47, alifariki akiwa anazuiliwa jela ambako alihukumiwa kifungo cha miaka 19 kwa makosa yanayoaminika kufungamana na ukaidi kwa utawala wa serikali ya Putin.

“Hakuna ubishi wowote, Putin ndiye amehusika na kifo cha Navalny,” akasema Rais Biden kwenye hotuba yake katika Ikulu ya White House Ijumaa.

Kifo cha Navalny, mmoja wa wakosoaji wakubwa zaidi wa Rais Putin ni pigo kwa juhudi za kidemokrasia, ambapo wanaopigania utawala huru wamekuwa wakifungwa na kuwindwa tangu Urusi ivamie Ukraine mnamo 2022.

Ingawa Navalny na wafuasi wake wengi walitarajia kuwa atauawa akiwa jela, ni wachache waliodhani inaweza kuwa punde namna hiyo.

Habari za kifo chake zimeibua hisia za majonzi na hasira miongoni mwa wafuasi wake, na familia yake.

“Sijui iwapo niamini habari hizi za kusikitisha,” akasema mkewe Yulia, wakati wa hotuba yake kwenye kongamano kuhusu usalama jijini Munich, Ujerumani.

“Lakini kama ni kweli, basi ningependa Putin, serikali yake na washirika wake kujua kwamba wataadhibiwa kwa kile walichofanyia taifa letu, familia yangu na mume wangu. Watafikishwa mbele ya haki hivi karibuni.”

Kifo cha Navalny kinaibua maswali kuhusu kile ambacho mataifa ya magharibi yanafaa kufanya ili kumkabili Putin, ambaye amewekewa vikwazo tangu 2022 na ameshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu kwa mauaji na utekaji wa watoto wa Ukraine.

Rais Biden mnamo 2021 aliahidi “hatua za kusambaratisha” kwa Urusi iwapo Navalny atafariki akiwa kizuizini. Lakini haijulikani ni nini haswa kitamzuia Putin dhidi ya kukamata na kuzuilia wengi wa wafuasi wa Navalny nchini Urusi na hata ughaibuni.

Katika matamshi yake ya punde, Biden alikuwa amempongeza Navalny kwa ujasiri wake wa kuamua kurejea Urusi licha ya kuwa ilikuwa dhahiri kwamba atakamatwa na kutupwa jela.

  • Imetafsiriwa na Fatuma Bariki